Habari za Kitaifa

Muda wa polisi wa Kenya nchini Haiti wafikia kikomo kikosi kipya cha kijeshi kikiundwa

Na NYABOGA KIAGE, DUNCAN KHAEMBA October 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UAMUZI wa Kenya kuongoza kikosi nchini Haiti chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa (UN) ulitajwa kuwa wa kihistoria na wenye ujasiri.

Kwa taifa lililokumbwa na ghasia za magenge, msukosuko wa kisiasa, na janga la kibinadamu, ulikuwa mwangaza wa matumaini.

Hata hivyo, jukumu hilo sasa limehitimishwa rasmi baada ya miezi 15, huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likipitisha azimio jipya lililowasilishwa na Amerika na Panama, kuanzisha Kikosi Maalum cha Kukabiliana na Magenge (Gang Suppression Force – GSF).

Kwa mujibu wa azimio hilo, idadi ya maafisa wa usalama wanaotarajiwa kupelekwa Haiti itaongezeka hadi 5,550, na muda wa chini wa kuhudumu utakuwa miezi 12.

Tofauti na kilichoongozwa na Kenya, kikosi hiki kipya kitaendeshwa kwa mujibu wa mamlaka rasmi ya Umoja wa Mataifa – jambo linalomaanisha kuwa sasa kitakuwa na ruhusa ya kutumia nguvu za kijeshi iwapo amani itatishiwa. Pia, ufadhili wake unatarajiwa kuwa wa uhakika zaidi.

Wiki iliyopita, Rais William Ruto alisisitiza kuwa licha ya changamoto maafisa wa Kenya waliweza kudhibiti uwanja wa ndege wa Port-au-Prince, kurejesha ikulu ya rais mikononi mwa serikali, na kufungua barabara muhimu kadhaa.

Hata hivyo, Rais Ruto alilalamikia ukosefu wa vifaa akisema kuwa kikosi hicho kilifanya kazi kwa chini ya asilimia 40 ya maafisa waliokuwa wameidhinishwa. Kati ya maafisa 2,500 waliopangwa, chini ya 1,000 waliweza kupelekwa Haiti.

Ujasiri wa Nairobi kujitolea katika mzozo ambao mataifa mengi ya Magharibi yaliepuka umetajwa na wachambuzi kama “mabadiliko ya mkondo wa kidiplomasia.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alisifu uamuzi huo akisema kuwa “kikosi hicho ni mfano halisi wa mshikamano wa kimataifa kwa vitendo.”

Katika taarifa yake ya jana, Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Kenya ilikaribisha azimio hilo la UN, ikisema kuwa ni ushahidi wa uongozi thabiti wa Kenya katika kuhamasisha jamii ya kimataifa, kushirikiana kwa makubaliano, na kuchochea hatua za pamoja, wakati wengine walipoona hatari.

“Uamuzi wa Kenya haukuchochewa na sifa, bali na misingi. Ushiriki wetu Haiti umejikita katika kulinda jamii dhaifu, kutekeleza Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na kushikilia amani ya kimataifa kwa mujibu wa wajibu wa kisheria wa kimataifa,” ilisema wizara.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alisema kuwa maafisa wa Kenya wamepata maarifa muhimu kupitia jukumu lao Haiti.

“Nimefurahi kuwa UN imepitisha azimio la kupanua kikosi. Hii itawezesha baadhi ya maafisa wetu kurejea nyumbani wakiwa na maarifa yatakayotusaidia kupambana na magenge hapa nyumbani. Tunajivunia kazi yao na sifa chanya ambayo Kenya imepata kimataifa,” alisema Murkomen.

Wakati wa jukumu hilo la miezi 15, maafisa watatu wa polisi wa Kenya walipoteza maisha, akiwemo Koplo Kennedy Mutuku Nzuve, aliyefariki katika ajali ya barabarani mnamo Septemba 1. Mwili wake ulirejeshwa Nairobi mwishoni mwa Septemba.