Kibarua cha usalama wanafunzi 3.4 milioni wakifanya mitihani ya kitaifa
Zaidi ya wanafunzi milioni 3.4 wanatarajiwa kuanza mitihani ya kitaifa kuanzia Oktoba 17, 2025, katika ratiba kubwa zaidi ya mitihani kuwahi kuandaliwa nchini, hatua inayoweka shinikizo kubwa kwa sekta ya elimu ya msingi pamoja na idara za usalama.
Kwa mara ya kwanza, mitihani itajumuisha Kenya Junior School Education Assessment (KJSEA) kwa wanafunzi wa Gredi 9. Jumla ya wanafunzi 1,130,669 wamesajiliwa kwa mtihani huu wa kwanza chini ya mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBE) na wanatarajiwa kujiunga na shule ya Sekondari Pevu Januari 2026.
Kwa mujibu wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Kenya (KNEC), Dkt David Njeng’ere, wanafunzi 996,078 wamesajiliwa kwa Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE), huku 1,298,089 wakijiandaa kwa tathmini ya Gredi 6 (KPSEA). Hii inafanya idadi kamili ya wanafunzi wanaofanya mitihani ya kitaifa mwaka huu kuwa 3,424,836, idadi kubwa zaidi katika historia ya mitihani ya kitaifa humu nchini.
Kutokana na idadi hiyo kubwa, serikali imelazimika kuhusisha maelfu ya maafisa wa usalama kuhakikisha usalama wa vifaa vya mitihani, usafirishaji wake pamoja na utulivu katika vituo vya mitihani.
“Katika miaka miwili iliyopita, tumefaulu kukabiliana na kuzuia changamoto ya uvujaji wa karatasi kufuatia karatasi zote mbili kupelekwa vituoni kwa wakati mmoja. Mfumo huu utaendelezwa mwaka huu,” alisema Dkt Njeng’ere wakati wa uzinduzi wa mchakato wa mitihani ya mwaka huu.
KNEC imeongeza idadi ya makontena ya kuhifadhi mitihani kutoka 617 mwaka jana hadi 642 mwaka huu, ili kuhakikisha vifaa vinawafikia wanafunzi kwa wakati.
Kwa KCSE, kutakuwa na wasimamizi wakuu 12,126, wasimamizi wa mtihani 54,782, mameneja wa vituo 10,765, madereva 2,692 na maafisa wa usalama 22,247.
Kwa KPSEA na KJSEA, idadi kubwa zaidi itahitajika huku wasimamizi wakuu wakiwa 26,479, wasimamizi wa mtihani wakiwa 125,492 na mameneja wa vituo 24,213.
“Katika KPSEA na KJSEA, maafisa wa usalama watatumika tu pale ambapo usalama ni changamoto. Lengo ni kuhakikisha mazingira ya kawaida na tulivu kwa wanafunzi hawa,” alifafanua.
]Ili kudhibiti udanganyifu, KNEC itaendeleza mfumo wa ambapo kila karatasi ya mtihani itakuwa na jina la mwanafunzi na nambari yake ya mtihani. Mwanafunzi atalazimika kusaini na kuweka tarehe katika karatasi yake na kwenye sehemu ambayo itakatwa na kuwekwa kwenye bahasha maalum baada ya kila mtihani.
“Hii inasaidia kuondoa upendeleo wakati wa usahihishaji na pia kudhibiti visa vya udanganyifu,” alisema Dkt Njeng’ere.
Pia alitangaza kuwa mwaka huu, KNEC itajaribu kutumia mbinu za kielektroniki kufunga makontena 250 ili kuimarisha usalama wa mitihani.
Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisisitiza umuhimu wa uaminifu na maadili wakati wa mitihani. Alionya kuwa yeyote atakayepatikana na hatia ya udanganyifu atachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Hatutakuwa na huruma kwa yeyote atakayehusika katika visa vya udanganyifu. Wanafunzi, wasimamizi na wakurugenzi wa mitihani lazima wazingatie kanuni zote,” alisema.
Aliongeza kuwa Sh950 milioni zimetengwa mwaka huu kuwapa walimu mafunzo ya kuendesha mfumo mpya wa elimu wa CBE kwa ufanisi.
Waziri Ogamba pia alisema kuwa KJSEA itatumika kama msingi wa kuwachagua wanafunzi kwa shule za sekondari pevu kulingana na mikondo mitatu ya taaluma : Sayansi na Teknolojia (STEM), Sayansi ya Jamii, na Sanaa na Michezo.
Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Huduma za Walimu (TSC), Bi Evaleen Mitei, aliwahimiza wazazi kuwasaidia wanafunzi kwa kuhakikisha mazingira utulivu na kuwapa motisha.
“Mitihani si vita wala ushindani. Ni nafasi ya wanafunzi kuonyesha walichojifunza na namna wanavyokua. Wazazi waepuke kuwatia watoto shinikizo lisilohitajika,” alisema.
Bi Mitei pia alitangaza kuwa maafisa wote wa TSC waliokuwa likizoni wamerejeshwa kazini ili kusaidia katika kusimamia mchakato wa mitihani.