Hofu upinzani kugawanyika Gachagua na Matiang’i wakirushiana maneno
Muungano wa United Opposition, uliokuwa ukipigiwa debe kama nguzo madhubuti ya kumpinga Rais William Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, sasa unaonekana kuyumba kutokana na mikwaruzano ya vinara wawili.
Chanzo kikuu cha hali hii ni tofauti za wazi kati ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, hasa kuhusu uhusiano wao na chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Jana, Bw Gachagua, alidharau siasa za ‘mikutano ya hoteli’ akisema haziwezi kufanya mtu kuwa Rais, huku akimshambulia Bw Matiang’i kwa kuendeleza siasa za ‘mezani’ badala ya kuzuru mashinani kukutana na wananchi.
“Hakuna Rais anayetengenezwa ndani ya chumba cha hoteli,” Gachagua alisema akiwa makao makuu ya chama chake cha Democracy for Citizens Party (DCP) jijini Nairobi.
“Uchaguzi unashinda au kushindwa mashinani. Njia ya kwanza ni mashinani, ya pili ni mashinani, ya tatu ni mashinani. Hakuna njia nyingine. Hauwezi kupakia picha mtandaoni ukijiita ‘Rais wa Sita’ na kudhani utachaguliwa.”
Kauli hizo zilielekezwa kwa Bw Matiang’i ambaye amekuwa akionekana kuegemea chama cha Jubilee. Aidha, alionekana kuwakejeli viongozi wenzake ndani ya upinzani wanaoamini umoja unaweza kuundwa kwa mikutano katika hoteli jijini.
“Wakenya wote wanajua kuwa ni DCP pekee inayowakilisha azma ya kumaliza utawala wa Ruto kwa muhula mmoja tu. Ndio maana mikutano yetu ndio hupigwa marufuku kila mara,” aliongeza Gachagua.
Jana Bw Matiang’i alisusia mkutano wa United Opposition huko Kajiado na badala yake akakutana na vijana katika Kaunti ya Nakuru, ambako alitetea uamuzi wake wa kushirikiana na Jubilee na kushikilia kwamba ana haki ya kuchagua chama chochote.
“Hauwezi kuchagulia mtu chama. Hauwezi kuniambia nani wa kushirikiana naye. Jubilee inajijenga upya, na mimi niko tayari kutembea safari hiyo,” alisema Matiang’i.
Kauli hiyo ilionekana kumjibu Gachagua aliyetaja DCP kuwa chama pekee cha upinzani katika eneo la Mlima Kenya. Bw Matiang’i pia alionekana kutetea ushawishi wa Rais mstaafu Kenyatta katika siasa za upinzani.
“Chama cha Jubilee kinapaswa kuwa chama kinachoongozwa na vijana,” alisema, akihimiza vijana kujisajili kupiga kura na kujitokeza kuwania nyadhifa kupitia chama hicho.
Tofauti hizo zimezua wasiwasi kwamba upinzani unaweza kugawanyika kwa misingi ya kikabila na kikanda. Bw Gachagua amemtaka Matiang’i “ajenge umaarufu wake Kisii” – kauli iliyotafsiriwa kama jaribio la kuwatenganisha wapinzani kwa misingi ya eneo wanakotoka.
Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, naye alimshtumu Gachagua kwa madai ya kushirikiana kwa siri na Rais Ruto. Alidai kuwa Gachagua alijigamba kuwa na kura milioni saba kutoka Mlima Kenya, milioni moja kutoka Kalonzo, na kura 800,000 kutoka kwa Matiang’i, kujisawiri kama mfalme mtarajiwa wa upinzani.
Lakini Gachagua alikanusha madai hayo na kusisitiza yeye ndiye mpinzani wa kweli wa utawala wa Ruto.
“Ni mikutano ya DCP pekee ndiyo inasambaratishwa na genge la wahuni. Ruto anajua sisi ndio tishio pekee la kweli,” alisema.
Wachambuzi wa kisiasa wanaonya kuwa mivutano hiyo ya ndani inaweza kuathiri vibaya juhudi za kuungana na kuwasilisha mgombea mmoja 2027. Huku Jubilee ikijaribu kujijenga upya, DCP ikipigania usemi mkubwa, na vyama kama Wiper, Narc-Kenya, na DAP-K vikionekana kutochukua msimamo thabiti.
Huku Gachagua akijionyesha kama mhanga wa mateso ya kisiasa, wapinzani wake wanamuona kama kikwazo anayependa kufanya maamuzi peke yake. Kwa upande mwingine, ushirikiano wa Matiang’i na Kenyatta unaonekana tishio kwa baadhi ya wanasiasa wanaotaka sura mpya katika upinzani.
“Safari hii itapima ukomavu wetu wa kisiasa, uwezo wa kujumuisha wengine, na ustahimilivu wetu,” alisema Matiang’i.