Habari za Kitaifa

Masaibu ya NG CDF yaongezeka ikidaiwa ushuru wa Sh2.2 milioni

Na SAMWEL OWINO October 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) inaendelea kukumbwa na changamoto nyingi huku Mamlaka ya Ukusanyaji Mapato Kenya (KRA) ikidai Sh2.2 bilioni kama deni la ushuru kutoka kwa bodi ya hazina hiyo.

Hazina hiyo inakumbwa na hatari ya kufutwa rasmi Juni mwaka ujao, huku KRA ikiwataka wasimamizi wake kulipa deni hilo la ushuru linalohusiana na baadhi ya maeneo bunnge tangu mwaka 2021.

Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Fedha za Miradi ya  Maeneo Bunge, mbunge wa Mwingi Kati, Gideon Mulyungi, aliibua suala hilo bungeni akisisitiza kuwa wasimamizi wa baadhi ya maeneo bunge walipokea barua kutoka KRA kuhusu deni hilo.

Mbunge Mulyungi alifahamisha Bunge kuwa maeneo bunge mengi yanayodaiwa hayakukubali kiasi kilichotajwa, lakini licha ya mazungumzo mengi kati ya bodi ya NG-CDF na KRA, suala hilo halijapatiwa ufumbuzi.

“Katika majadiliano mengi kati ya bodi ya NG-CDF na KRA, bado matatizo haya yameendelea kuwepo,” alisema Mulyungi.

Kulingana na KRA, hadi Mei 31, 2025, maeneo bunge mbalimbali yanadaiwa jumla ya Sh2.2 bilioni.

Mbunge huyo sasa anataka Bunge kupitia Kamati ya Fedha na Mipango ya Kitaifa, inayosimamiwa na mbunge wa Molo, Kimani Kuria, kuandaa kikao na KRA ili kupata ufafanuzi wa hali halisi ya deni la kila eneo bunge  na maelezo kamili ya kiasi linalodaiwa.

Aidha, Mulyungi anataka kamati hiyo ipate taarifa kuhusu hatua za wazi zinazochukuliwa na KRA na bodi ya NG-CDF kutatua tatizo hili pamoja na muda wa makubaliano ya kulipa madeni hayo.

Matakwa mapya ya KRA yanaongeza matatizo yaliyokumba hazina hiyo, huku ikisubiriwa kufutwa rasmi Juni 30, 2026, kama ilivyoagizwa na Mahakama.

Wiki iliyopita, wabunge walionyesha wasiwasi kuwa wasimamizi wa hazina bado hawajapokea mgao wa kwanza wa Sh19 bilioni kutoka Wizara ya Fedha.

Wabunge walihofia kuwa kama hakuna hatua itakayochukuliwa kabla ya Juni 30, 2026, hazina hiyo itaachwa madeni ya zaidi ya Sh50 bilioni, jambo litakalosababisha miradi mingi kusimama kwani wasimamizi wameshafanya mikataba na wakandarasi.

Wizara ya Fedha iliahidi bungeni kutoa jumla ya Sh58 bilioni kwa maeneo bunge yote  kabla ya Juni 30, 2026, huku kila ka moka likitarajiwa kupokea angalau Sh7 bilioni kila mwezi kuanzia mwezi huu.

Tangu hazina hiyo iharamishwe na Jopo la Majaji watatu mwaka jana, wabunge wamechukua hatua mbalimbali kuhakikisha inaungwa mkono na katiba ili kuzuia kufutwa kwake.

Bunge limepitisha Mswada wa Marekebisho ya Katiba ya Kenya, 2025, unaolenga kuweka hazina tatu muhimu katika katiba.

Mswada huo unaoungwa mkono na mbunge wa Rarieda, Otiende Amollo, na mwenzake wa Ainabkoi, Samuel Chepkonga, unalenga kuweka Hazina ya Maendeleo ya Kaunti za Serikali Kuu (NG-CDF), Hazina ya Uangalizi ya Seneti (SOF), na Hazina ya Usawa ya Serikali Kuu (NG-AAF) katika katiba.