Makala

Rais wa Madagascar Rajoelina apuuza wito wa kujiuzulu

Na REUTERS, WINNIE ONYANDO October 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS wa Madagascar, Andry Rajoelina, amesema kuwa yuko tayari kwa mazungumzo ya kutafuta suluhu la matatizo yanayolikabili taifa.

Hata hivyo, kiongozi huyo amepuuza kabisa wito wa kujiuzulu kwake kutokana na vuguvugu la maandamano linaloongozwa na vijana nchini kote.

Kwa kuchochewa na maandamano kama hayo ya “Gen Z” nchini Kenya na Nepal, maandamano hayo yameongezeka tangu wiki iliyopita na kuwa wimbi kubwa zaidi la machafuko ambalo Madagascar limeshuhudiwa kwa miaka mingi, na kuibua kutoridhika na viwango vya juu vya umaskini na ufisadi.

Rais huyo aliamua kukaa kando kidogo ili kuruhusu mazungumzo lakini hatua hiyo haijaleta suluhu kabisa kwani wananchi wameendelea kuonyesha kutoridhishwa kwao na uongozi wake.

Umoja wa Mataifa unasema takriban watu 22 waliuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika siku chache za kwanza za maandamano hayo, takwimu ambao serikali ilikana.

“Hakuna anayefaidika na uharibifu wa taifa. Niko hapa, nimesimama hapa tayari kusikiliza, tayari kuleta suluhisho kwa nchi yetu,” Rajoelina alisema katika hotuba iliyotangazwa kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Alisema, bila ya kutoa Ushahidi kuwa kuna baadhi ya wanasiasa walikuwa wakipanga njama za kujinufaisha na maandamano hayo na wamefikiria kufanya mapinduzi.

Kiongozi huyo alisema hayo alipokuwa akihutubia Umoja wa Mataifa mjini New York wiki iliyopita.

“Ukosoaji wa matatizo yaliyopo si lazima uonyeshwe mitaani; unapaswa kufanywa kwa njia ya mazungumzo,” alisema Rajoelina, ambaye aliingia madarakani kwa mara ya kwanza katika mapinduzi ya mwaka 2009 baada ya kuongoza maandamano makubwa dhidi ya serikali.

Katika chapisho kwenye mtandao wake wa kijamii wa X siku ya Ijumaa Oktoba 3, 2025, Rajoelina alisema pia amekutana na makundi mbalimbali kwa siku tatu zilizopita ili kuzungumzia hali hiyo.

Maandamano yalianza tena katika mji mkuu Oktoba, 3, 2025 baada ya kusimama kwa siku moja, huku polisi wakifyatua vitoa machozi kuwatawanya baadhi ya waandamanaji, kanda za runinga ya Real TV Madagasikara zilionyesha.

Licha ya Madagascar kuwa na utajiri mkubwa wa madini, taifa hilo ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani.