Jamvi La Siasa

Gideon sasa arejea kufufua ushawishi wa Moi Bondeni

Na BENSON MATHEKA October 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UAMUZI wa Gideon Moi kugombea kiti cha Seneta wa Baringo katika uchaguzi mdogo wa Novemba 27, unaonekana kama hatua ya kuokoa jina na ushawishi wa kisiasa wa familia ya Moi, ambalo lilizimwa na wimbi la chama tawala cha UDA mwaka wa 2022.

Mnamo Alhamisi, Gideon, ambaye ni mwanawe rais wa pili wa Kenya, hayati Daniel arap Moi, alitangaza rasmi kuwa atawania kiti hicho kupitia chama cha KANU – ambacho pia anahudumu kama mwenyekiti wake.

Tangazo lake lilijiri baada ya kimya cha muda na uvumi kuhusu mustakabali wake kisiasa.Hatua hii inaashiria jaribio la wazi la kurudisha heshima ya kisiasa ya familia ya Moi, hasa katika ngome yao ya muda mrefu ya Baringo, ambayo sasa imekuwa uwanja wa vita kati ya urithi wa KANU na nguvu ya chama tawala cha UDA kinachoongozwa na Rais William Ruto.

Hayati Moi alivuma katika siasa za eneo hili kwa zaidi ya miaka 50 akiwa rais na mbunge wa Baringo ya Kati.Katika uchaguzi wa 2022, Gideon alipoteza kiti hicho kwa marehemu William Cheptumo wa UDA, huku kaka yake, Raymond Moi, naye akishindwa katika eneobunge la Rongai.

Huo ulikuwa mwanzo wa kuporomoka kwa ushawishi wa familia hiyo ambayo kwa miaka mingi ilitawala siasa za Bonde la Ufa.Kifo cha Cheptumo mwezi Februari 2025 kilifungua nafasi mpya ya uchaguzi, na sasa Gideon anajitosa uwanjani kwa matumaini ya kurejesha ushawishi wa familia yake, akilenga kuchuma nafuu kutokana na hasira za wananchi dhidi ya serikali iliyochochewa na maandamano ya vijana wa Gen Z mwaka jana.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, ikiwa Gideon atashinda, basi ushindi huo utatafsiriwa kuwa kura ya kutokuwa na imani na uongozi wa Rais Ruto katika ngome yake mwenyewe ya kisiasa na kufufua ushawishi wa familia ya Moi uliozimwa na umaarufu wa Rais Ruto.

Kwa upande mwingine, Rais Ruto ameonyesha kuvalia njuga mapambano haya. Tayari amemteua mjane wa Cheptumo, Bi Hannah Wendot, kuwa Waziri wa Masuala ya Jinsia – uteuzi unaotajwa kuwa mbinu ya kujihakikishia uungwaji mkono kutoka kwa familia ya Cheptumo na wakazi wa Baringo.

Wanaounga mkono serikali wameanza kutumia uteuzi huo kama silaha ya kisiasa, wakisema Rais aliwajali wakati wa majonzi na hivyo basi anastahili kuendelea kuaminiwa.

Mbunge wa Tiaty, William Kamket aliyewahi kuwa mshirika wa karibu wa Gideon Moi sasa ni mmoja wa sauti kali za kumpinga Gideon, akisisitiza kuwa ni mgombea wa UDA pekee atakayeungwa mkono na wakazi wa Baringo.“Kiti cha seneta wa Baringo kitaenda kwa UDA.

Kama hauko UDA, potea!” alinukuliwa akisemaKatika taarifa rasmi ya Oktoba 2, KANU ilithibitisha kuwa Mwenyekiti wao Gideon Moi atakuwa mgombea rasmi wa chama hicho. Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama, Manasse Nyainda, alisema uteuzi huo uliafikiwa baada ya “mashauriano ya kina” kati ya chama na watu wa Baringo.“Tuna imani kuwa rekodi ya Moi ya uongozi na maono ya maendeleo yataungwa mkono na wananchi,” alisema Nyainda.

Aliongeza kuwa kampeni ya Moi itajikita katika sera, uwajibikaji na ushirikishaji wa wananchi.Katika uchaguzi wa mwisho, Gideon alipata kura 71,480 dhidi ya Cheptumo aliyepata 141,777.

Mara hii, Gideon anatarajiwa kupambana na Vincent Chemitei wa UDA na mgombea huru Benjamin Chebon.Sasa, macho yote yameelekezwa Baringo kuona ikiwa Gideon atafufua nyota ya kisiasa ya familia ya Moi, au wimbi la UDA litaendelea kufagia kila kona ya Bonde la Ufa.