Utaondoka na ulichochangia katika ndoa ikivunjika
Sheria ya Mali ya Ndoa ya mwaka 2013 ndiyo sheria kuu inayotoa mwongozo wa jinsi mali ya ndoa inavyopaswa kugawanywa baada ya talaka nchini Kenya.
Sheria hii inafafanua mali ya ndoa kuwa ni nyumba ya familia, vifaa vya nyumbani vilivyomo humo, mali yoyote inayohamishika au isiyohamishika iliyopatikana kwa pamoja wakati wa ndoa.
Mali iliyowekwa chini ya mkataba wa awali wa ndoa au iliyoko kwenye amana haijumuishwi.
Kifungu cha 2 kinafafanua mchango kuwa ni wa kifedha au wa kawaida (usio wa pesa), ikiwa ni pamoja na kazi za nyumbani, kulea watoto, usimamizi wa biashara au mali ya familia, kazi ya shamba na kuwa mpenzi anayetoa usaidizi.
Kifungu cha 6 kinaeleza kuwa mali ya ndoa ni ile iliyopatikana wakati ndoa bado ipo, na inajumuisha nyumba ya familia, mali ya nyumbani, na mali yoyote iliyopatikana kwa pamoja kwa faida ya wote wawili.
Kifungu cha 7 kinaweka bayana kuwa umiliki wa mali ya ndoa hutegemea mchango wa kila mmoja, iwe wa pesa au wa kawaida.
Kifungu cha 9 kinatambua michango ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja, kama vile kazi za nyumbani, kulea watoto, kazi ya shambani, na kuboresha mali.
Kifungu cha 14 kinaangazia mali ya ndoa iliyosajiliwa kwa jina la mume au mke mmoja. Kuna dhana inayoweza kupingwa kwamba mali hiyo inashikiliwa kwa niaba ya mwenzi wake. Ikiwa mali imesajiliwa kwa majina ya wote, kuna dhana ya umiliki wa nusu kwa nusu hadi ithibitishwe vinginevyo.
Kifungu cha 17 kinampa mume au mke haki ya kuomba mahakamani apewe haki yake kuhusu mali iliyopatikana wakati wa ndoa ambayo umiliki wake unazozaniwa.
Mahakama za Kenya zimekuwa zikifafanua vifungu vya sheria hii kwa kuzingatia mazingira ya ndoa na michango ya wahusika.
Katika kesi ya Joseph Ombogi Ogentoto dhidi ya Martha Bosibori (2023) Mahakama iliamua kuwa ugavi wa mali ya ndoa hauwi wa nusu kwa nusu moja kwa moja baada ya talaka.
Ingawa Katiba ya Kenya, Ibara ya 45(3), inahakikisha usawa wa haki kwa wanandoa wakati wa ndoa na wakati wa kuvunjika kwake, usawa huu haujaweka moja kwa moja haki ya kugawana mali kwa nusu.
Kila mume au mke ana haki ya kupata kile alichochangia kwa njia ya kifedha au kwa njia isiyo ya kifedha. Mahakama ilisisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kuondoka na kile alichopata kwa juhudi zake binafsi.