Sababu za matineja wa Gen Z kukosa kuonyesha hisia kwa picha
Tabia ya vijana wa kizazi cha Gen Z kupiga picha au video wakiwa na uso usio na tabasamu wala hisia—inayojulikana kama “Gen Z stare” imeanza kuvutia hisia kutoka kwa watafiti wa utamaduni na saikolojia.
Ingawa haijafanyiwa utafiti wa kina wa kisayansi, tafiti zinazohusiana zinaonyesha kuwa hali hii inaweza kuakisi masuala ya malezi kama vile utambulisho, mwonekano, udhibiti wa hisia, na jinsi mtu anavyojiwasilisha mtandaoni.
“Gen Z stare” hujumuisha kutazama moja kwa moja kamera bila kupepesa macho wala tabasamu. Tofauti na vizazi vya awali vilivyopendelea kuonekana wachangamfu au wakifurahia maisha, vijana wengi wa Gen Z huonekana kupendelea uso usio na hisia yoyote—hali ambayo inaweza kuonekana kama mzaha, ukweli, au vyote viwili kwa pamoja.
Nini kinaweza kusababisha hali hii?
kulingana na mwanasaikolojia Dkt Tara Well, tafiti zinaonyesha kuwa uso usio na hisia unaweza kusaidia mtu kujizuia kuonyesha hisia zake hadharani.
“Kwa Gen Z, hofu ya kuonekana kuwa “wanajitahidi kupita kiasi” au kuonekana wa kuchekesha huwachochea kudhibiti hisia zao wakiwa mtandaoni, kama njia ya kuonyesha kuwa wanajidhibiti,” asema.
Watafiti wa saikolojia ya mitandao wanasema kuna mabadiliko ya kizazi kutoka kujionyesha kama watu wa kuvutia hadi kuonekana wa kawaida au waliokosa hisia. Kwao, kupiga picha bila tabasamu ni njia ya kukataa utamaduni wa “cheka kwa kamera” uliozoewa na Millennials na Gen X.
“Gen Z walikua wakitazama picha na video zisizoisha mtandaoni. Uso wao wa kukosa hisia huweza kuonyesha kuchoka kwao au kutoathirika kihisia, hali ambayo wataalamu wanaiita affective flattening—yaani kupungua kwa uwezo wa kuonyesha au kuhisi hisia baada ya kuzoea msisimko mwingi wa kidijitali,” asema Tara.
Tofauti na picha zilizopigwa kwa mtindo wa “Instagram face,” uso wa Gen Z hukataa vigezo vya urembo vilivyozowa. Wanapendelea kuonyesha hali halisi, hata ikiwa ni hali ya kutojali, kutoeleweka au hata kuwa na aibu. Wataalamu wa urembo wanasema hii ni aesthetic of resistance.
Kwa vijana wengine, Gen Z stare ni ishara ya kuelewa mzaha wa maisha ya mtandaoni, hasa wanapoambatanisha picha hizo na maneno ya kuchekesha.
Kwa ujumla, asema Tara, jicho la Gen Z si jicho tu—ni ujumbe mzito. Linaonyesha mabadiliko ya mitazamo kuhusu uhalisia, umaarufu mtandaoni, na pia linaweza kuwa njia ya kuweka mipaka ya kihisia katika ulimwengu ambao mambo yanaanikwa kupita kiasi.