Wanne wafariki, 30 watibiwa kutokana na mkurupuko wa kipindupindu
WATU wanne wamethibitishwa kuaga dunia na wengine zaidi ya 30 wanaendelea kupokea matibabu hospitali mbalimbali Kaunti ya Narok baada ya kupatikana na kipindupindu.
Afisa Mkuu wa Huduma za Afya Narok Lucy Kashu alithibitisha mkurupuko wa kipindupindu katika wadi za Kilgoris ya Kati, Shankoe na Lolgorian kwenye kaunti ndogo za Trans Mara Magharibi na Kusini.
Vipimo vilivyofanywa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Trans Nzoia Magharibi na maabaara ya Walter Reed, Kericho vilithibitisha maambukizi ya kipindupindu mnamo Oktoba 3.
“Kufikia Ijumaa, wagonjwa 12 ambao watano ni wanaume watano wengine wanawake pamoja na watoto wawili bado walikuwa wamelazwa. Wengine 15 nao wametibiwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani,” akasema Bi Kashu.
Mauti yalikuwa ya watu watatu wazima na mtoto mmoja kutoka vijiji vya Migingo, Majengo na Oldonyo Rasha.
“Kaunti inawahakikishia raia kuwa vitengo vyake vikiwemo vile vya kutoa huduma za dharura kwenye maeneo ambayo yameathirika, viko sawa,” akasema Bi Kashu.
Aliongeza kuwa kituo cha dharura cha kutibu kipindupindu kimeanzishwa Hospitali ya Trans Mara Magharibi kama mojawapo ya juhudi za kuzuie kuenea kwa ugonjwa huo unaoangamiza kwa haraka.
Maafisa wa afya nao wanaendelea na uchunguzi wao pamoja na mahamasisho kisha pia wanafanya kwa karibu na asasi mbalimbali kuhakikisha wakazi wanatumia maji safi.
“Kipindupindu huwa kinaenea kwa sababu ya uchafu na unywaji wa maji yasiyo safi. Tunawashauri wakazi wadumishe viwango vya juu vya usafi, wayatibu maji ya kunywa na wasake matibabu iwapo wanashuku wana dalili za kipindupindu,” akaongeza Bi Kashu.
Serikali ya kaunti imetoa wito kwa umma ushirikiane nao wakifanya kazi pamoja na serikali ya kitaifa kupitia idara ya afya kuzima kipindupindu.
Afisa huyo pia aliwataka wakazi wapige ripoti kuhusu kisa chochote cha kuendesha na kutapika kwa maafisa wa afya.
Maafisa wa afya pia wanatathmini kupiga marufuku uchuuzaji wa vyakula katika maduka na maeneo ya karibu kudhibiti kipindupindu kinachoenea kwa haraka sana.