Marais 2 pekee wahudhuria kuapishwa kwa Mutharika baada ya kumfanya Chakwera ‘Wantam’
BLANTYE, Malawi
MARAIS wengi wa mataifa ya Afrika Jumamosi, Oktoba 4, 2025 walisusia sherehe ya kuapishwa kwa Peter Mutharika kuwa rais wa Malawi baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika Septemba 16, 2025.
Kulingana na vyombo wa habari nchini humo, ni marais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe na mwenzake wa Msumbiji Daniel Chapo walihudhuria hafla hiyo iliyoandaliwa katika uwanja wa michezo wa Kamuzu, jijini Blantyre.
Aidha, Rais anayeondoka Lazarus Chakwera hakuhudhuria sherehe hiyo, ila chama chake Malawi Congress Party kilituma ujumbe wa heri njema.
Profesa Mutharika, 85, aliyehudumu kama Rais wa Malawi kuanzia 2014 hadi 2020, alishinda kwa kupata asilimia 56 ya kura huku Chakwera akipata asilimia 33 na kupoteza ndoto yake ya kuhudumu muhula wa pili.
Mutharika anaingia afisini wakati ambapo Malawi inakabiliwa na changamoto za kiuchumi.
Kupanda kwa gharama ya maisha na uhaba wa mafuta na chakula ni baada ya changamoto zilizosababisha raia wa Malawi kukerwa na utawala wa Chakwera.
Malawi ambayo hutegemea kilimo, pia iliathirika na mabadiliko ya hali ya anga, zikiwemo kimbunga kilichotokea mwaka wa 2023 na ukame ulioharibu mazao ya shambani.
“Taifa letu linakabiliwa na changamoto. Kuna uhaba mkubwa wa chakula na pesa za kigeni. Hizi ni changamoto zilizosababishwa na binadamu,” Profesa Mutharika akasema katika hotuba yake baada ya kuapishwa.
“Tutasuluhisha changamoto hizi. Siwaahidi maziwa na asali, bali kazi kwa bidii,” akaongeza.
Mutharika alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwekeza nchini Malawi akiahidi kupambana na jinamizi la ufisadi.