Habari

Wazazi wa Litein Boys kulipa Sh69 milioni baada ya mgomo

Na VITALIS KIMUTAI October 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZAZI wa Shule ya Wavulana ya Litein Kaunti ya Kericho watalipa Sh69 milioni kama faini ili kugharimia uharibifu wa mali ya shule kutokana na mgomo uliozuka majuzi shuleni humo.

Faini hiyo imewashangaza wazazi wengi baadhi wakijiuliza watapata hela hizo wapi.

Hata hivyo, kutokana na rufaa iliyowasilishwa na Muungano Wazazi na Walimu, Bodi Simamizi ya shule (BOM) sasa itagharimia Sh30 milioni ya uharibifu mzima huku wazazi wakilipa Sh69 milioni.

Imebainika kuwa uharibifu mzima uliotokea ulikuwa Sh99,962,450 na wazazi ndio watahimili gharama kubwa huku bodi ikilipa kwa awamu pesa zilizosalia.

Bodi inatarajiwa kutuma ombi kwa serikali ikiwemo Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (CDF) kugharimia ukarabati. Upungufu wowote ambao utabaki utaangushiwa wazazi waugharimie.

Uamuzi wa kutoza wazazi Sh69 milioni uliafikiwa kutokana na mkutano kati ya mwenyekiti wa Bodi Dkt K. Kembo na mwenyekiti wa PTA Abadnego Rotich na maafisa wa Wizara ya Elimu.

Wahandisi kutoka Idara ya Serikali inayosimamia miundomsingi iliwasilisha ripoti yake ya ukaguzi kuhusu kiwango cha uharibifu uliotokea na makadirio ya bajeti ya kukarabati shule.

Kila mwanafunzi kati ya wanafunzi 1,400 atalipa Sh49,000 kugharimia ukarabati huo ambao ndio ghali zaidi kwenye historia ya migomo nchini.

“Gharama nzima ya uharibifu ni Sh69,578,795. Kiwango hicho kikigawanywa na kila mwanafunzi kati ya wanafunzi wote 1400 ni Sh49,699,” BOM ikasema kwenye ujumbe kwa wazazi.

Bodi ilisisitiza kuwa pesa hizo lazima zilipwe kwenye benki ya shule kufikia Oktoba 6 ili ukarabati uanze kabla ya wanafunzi kuruhusiwa kurejea shuleni.

PTA awali ilitaka kila mwanafunzi alipe Sh10,000 lakini ikabainika kiwango cha uharibifu kilikuwa juu mno.

Wanafunzi wa Kidato cha Pili watarejea shuleni Oktoba 9, wale wa Kidato cha Tatu Oktoba 13 kisha wa Kidato cha Nne Oktoba 16.

“Imeamuliwa kuwa wanafunzi wa Kidato cha Pili na Tatu watabeba mikoba yao na malazi huku wale wa Kidato cha Nne wakibeba kila kitu wanachohitaji,” akasema Mwalimu Mkuu Richard Sang’ ambaye pia ni katibu wa bodi simamizi ya shule.

Bodi pia ilikubaliana na Wizara ya Elimu kwamba deni lote la karo lazima limalizwe kabla mwanafunzi kuruhusiwa kurejea shuleni.

“Kila mwanafunzi lazima aandamane na mzazi na mkutano na wazazi utaitishwa hivi karibuni,” ikasema ujumbe kwa wazazi.

Uharibifu huo wa mali uliwaacha wazazi na washikadau katika sekta ya elimu na mshangao mkubwa.

Wanafunzi wanane tayari wamekamatwa na kufikishwa kortini na wanaendelea kuzuiliwa hadi uchunguzi unaoendeshwa na makachero kutoka Idara ya Upelelezi ukamilike.