Habari za Kitaifa

IEBC yamulikwa kuhusu teknolojia itakayotumia 2027 wakati ambapo AI inavuruga mambo

Na ERIC MATARA October 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MPANGO wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wa kutumia teknolojia mpya katika uchaguzi mkuu wa 2027 umeibua mjadala mkali miongoni mwa Wakenya na viongozi wa kisiasa, kufuatia hofu kuhusu usalama wa data na uadilifu wa mifumo hiyo.

Mwanaharakati kutoka jijini Nakuru, Laban Omusundi, ameandikia barua IEBC kuiomba iainike hali ya usalama ya mifumo yake, akionya kwamba teknolojia yake inaweza kuwa rahisi kuvurugwa na programu hasidi au kudhibitiwa na akili unde (AI).

Ombi lake linataka tume hiyo kuchapisha mfumo wa kina wa usalama wa mtandao ndani ya siku 60, kuanzisha ushirikiano na wataalamu wa kimataifa, na kuruhusu ukaguzi huru wa teknolojia za uchaguzi kabla, wakati, na baada ya kura.

Viongozi wa serikali na upinzani vilevile wametaka uwazi katika matumizi ya teknolojia ya uchaguzi. Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, alisema kuwa, ingawa teknolojia inaweza kuimarisha haki, haipaswi kuhatarisha demokrasia, akisisitiza kwamba uchaguzi lazima uakisi matakwa ya wananchi.

Hivi majuzi, IEBC ilizindua zoezi la kujiandikisha kwa wapiga kura likilenga kusajili wapiga kura wapya milioni 6.3, hasa vijana ili kuongeza idadi ya wapiga kura hadi milioni 28.5 kufikia 2027.

IEBC imefichua kuwa inatumia teknolojia ya Iris (upigaji picha wa mboni ya jicho) katika vifaa vya KIEMS, maboresho ambayo yanagharimu takriban Sh7 bilioni.

Kulingana na mtaalamu wa teknolojia na mawasiliano wa IEBC, Godfrey Ngunyi, teknolojia hiyo ya Iris inahakikisha usahihi wa hali ya juu kwa sababu mboni ya jicho la binadamu hubakia thabiti kwa muda mrefu, tofauti na alama za vidole ambazo hubadilika kutokana na kazi za mikono.

Hata hivyo, wataalamu wameibua wasiwasi kuhusu faragha na usalama wa mitandao. Mtaalamu wa usalama wa mtandao, Thomas Chiteri, ametaka IEBC kushirikiana na Ofisi ya Kamishna wa Ulinzi wa Data ili kulinda data zinazokusanywa wakati wa usajili, akionya kuhusu hatari kubwa ikiwa data hiyo itadukuliwa.

Wasiwasi wa umma bado ni mkubwa kufuatia hitilafu za vifaa vya KIEMS katika chaguzi za 2017 na 2022.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon, alihakikishia umma kwamba mifumo ya uchaguzi ya 2027 haitaingiliwa na kuwa itakuwa salama, ikiwa na ulinzi imara wa kiutawala na kiteknolojia ili kuhakikisha uchaguzi wa kuaminika.

Aliongeza kuwa mfumo wa KIEMS ulioboreshwa una moduli mpya ya usajili wa wapigakura kwa njia ya kibayometria, ili kuongeza kasi na ufanisi.

Ombi la Omusundi lilipokelewa na IEBC mnamo Septemba 23, 2025. Linasisitiza haja ya uwazi, ufuatiliaji wa moja kwa moja, na uchapishaji wa ripoti za umma baada ya matukio yoyote ya kiusalama.

Alionya kuwa hofu ya kuingiliwa kwa njia ya kidijitali inaweza kufifisha uadilifu wa demokrasia ikiwa haitashughulikiwa.

Wakati uo huo, wachanganuzi wa siasa wanatabiri kuwa wapiga kura wa kizazi cha Gen Z, wanaokadiriwa kufikia milioni 14, wanaweza kuwa na ushawishi mkubwa katika uchaguzi wa 2027.

Mnamo 2022, kutojitokeza kwa vijana kulichangia idadi ndogo ya wapiga kura. Ni wapiga kura milioni 14.3 pekee kati ya milioni 22.1 waliosajiliwa walijitokeza kupiga kura.

Wapiga kura wapatao milioni 7.8, wengi wao wakiwa vijana, hawakupiga kura. Ni jambo ambalo wachambuzi wa kisiasa walitaja kama chanzo kikuu cha kutojitokeza kwa wapiga kura.

Uchaguzi huo uliamuliwa kwa tofauti ya kura 200,000 pekee ambapo Rais William Ruto alizoa kura 7,176,141 na mpinzani wake wa karibu, aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, akipata kura 6,942,930.

Sasa, IEBC inatarajia teknolojia na mikakati yake ya uhamasishaji itarejesha imani ya umma na kuhamasisha ushiriki mkubwa wa vijana katika kuunda mustakabali wa kidemokrasia wa Kenya.