Habari

Vikao vya Seneti Mashinani vyaanza Busia

Na MARY WANGARI October 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

AWAMU ya nne ya ‘Seneti Mashinani’ imeng’oa nanga rasmi hii leo katika Kaunti ya Busia ambapo Bunge la Seneti  litaendesha vikao vyake kwa wiki moja katika Bunge la Kaunti ya Busia.

Spika wa Bunge la Seneti, Amason Kingi anayeongoza Kamati ya Shughuli za Bunge, alisema vikao hivyo  vinakusudiwa kuimarisha mtagusano kati ya Seneti na serikali za kaunti ikiwemo kuleta uwiano kati ya serikali kuu na serikali za kaunti.

Vikao hivyo vitakavyofanyika Busia vimejiri kufuatia uamuzi wa Kamati ya Shughuli za Seneti kutokana na  uamuzi uliofanywa na Seneti mnamo Machi 8, 2023, wa kuendesha vikao vya kamati katika kaunti kwa wiki moja kila Oktoba isipokuwa katika mwaka wa uchaguzi.

Kulingana na Spika Kingi,” Seneti Mashinani itawawezesha Wakenya kuelewa vyema wajibu wa bunge katika kufanikisha ugatuzi.”

Bunge limeorodhesha shughuli mbalimbali za kisheria zitakazofanyika wiki hii kando na vikao vya kawaida. Maseneta wataendesha ushirikishaji wa umma kuhusu Mswada wa Kufanyia Marekebisho Katiba, 2025, unaolenga kuimarisha wajibu wa seneti katika  uundaji sheria na uangalizi.

Kamati za Bunge zitaendesha vikao vyake kote kaunti hiyo na kuwapa wakazi fursa ya kushiriki shughuli za seneti kuhusu uundaji sheria, kuzuru miradi ya maendeleo, kukagua mipango ya serikali ikiwemo mikutano ya hadhara ambapo raia, wanaharakati na maafisa eneo hilo watatagusana moja kwa moja na maseneta.

Usimamizi wa Kaunti ya Busia unaoongozwa na Gavana Paul Otuoma utakutana na Kamati ya Seneti kuhusu Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (CPAC) inayoongozwa na Seneta Moses Kajwang (Homabay) kudadisi rekodi za kifedha katika bajeti ya 2023/2024.

Kamati nyinginezo zitakazoshiriki vikao vyake katika Bunge la Kaunti ya Busia ni pamoja na Kamati ya Seneti itakayodadisi utekeleezaji wa sheria kuhusu Elimu ya Chekechea na Vituo vya Kiufundi na Kamati ya Sheria itakayoshirikisha umma kuhusu Mswada wa Marekebisho kuhusu Katiba 2025.

Kamati nyinginezo zitakazoshiriki vikao vyake katika Bunge la Kaunti ya Busia ni pamoja na kamati za Kilimo, Biashara na Viwanda na Uwiano Kitaifa.

Karani wa Bunge la Seneti Jeremiah Nyegenye alisema vikao hivyo vinanuiwa kuendeleza wajibu na kazi ya seneti ikiwemo kukuza uhamasishaji wa umma kuhusu shughuli za seneti na bunge la kitaifa kwa jumla, ili kumulika pengo zilizopo na fursa mpya za kubuni na kuimarisha ushirikiano katika kiwango cha kaunti na serikali.

“Seneti mashinani inakusudia kuendeleza kazi ya Seneti na kuimarisha uhamasishaji kuhusu Shughuli za Seneti na Bunge kwa jumla na kutoa fursa kwa wanakamati na wafanyakazi wa bunge za kaunti kujifunza na kushiriki mbinu bora na maseneta na maafisa wa bunge,” alisema Bw Nyegenye.