Habari za Kaunti

Ruku anadi miradi ya serikali Mbeere akipigia debe mwaniaji wa UDA

Na GEORGE MUNENE October 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku , amesema serikali ya Kenya Kwanza inamakinikia miradi ya maendeleo kwa usawa ikiwemo katika maeneo ambayo yamebaguliwa kama Mbeere Kaskazini.

Eneobunge la Mbeere Kaskazini litakuwa na uchaguzi mdogo mnamo Novemba 27 na mrengo wa serikali unampigia debe Leonard Muthende.

Bw Ruku ambaye alikuwa akiongea wakati wa hafla ya mchango katika eneo la Makung’uru, alisema serikali ishatangaza tenda ya kukarabatiwa kwa Barabara ya Gikuyari-Kirii-Ishiara.

“Hii barabara imetumika kama ajenda ya kisiasa kwa kipindi kirefu lakini sasa chini ya serikali ya Kenya Kwanza tutaikarabati. Kutangazwa kwa tenda ya ujenzi wa barabara hii ni hatua kubwa katika kubadilisha eneo hili,” akasema Bw Ruku.

Alisisitiza kuwa Kenya Kwanza inamakinikia maeneo ambayo kihistoria yamebaguliwa kama njia ya kuhakikisha usawa katika kusambaza rasilimali za taifa.

“Serikali zilizopita zilibagua maeneo haya lakini sasa tunaona maendeleo. Tumakinike na kuendeleza safari ya kukumbatia mageuzi,” akaongeza.

Wakati wa hafla hiyo katibu huyo alikabidhi uongozi wa shule hiyo jengo jipya ambalo litakuwa na afisi za walimu.

Waziri huyo alisema kuwa elimu ndiyo silaha ambayo inahakikisha usawa kwa kila mtu nchini.

“Tunafanya kazi ili kuhakikisha kila mtoto anapata elimu wakiwemo wale ambao wanatoka maeneo kame,” akasema.

Alimpigia debe Bw Muthende akimrejelea kama kiongozi ambaye anaweza kuendelea na kazi ambayo alianza alipokuwa mbunge kabla ya kuchaguliwa waziri.

Alitaja mpango wa Imarisha Elimu Bora na miundomsingi kama miradi ambayo alianzisha na inayostahili kukamilishwa na mbunge atakayechaguliwa Novemba 27.

“Tulifanya kazi nyingi nilipokuwa mbunge wenu. Leonard Muriuki Muthende ndiye mtu ambaye anaweza kuendeleza kazi ambayo tulianzisha,” akasema Bw Muriuki.

Waziri huyo alimwagia maji kampeni ambazo zimekuwa zikiendelezwa na aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na Seneta wa zamani Lenny Kivuti Mbeere Kaskazini akisema hazitawashawishi wakazi kumchagua mwaniaji wa upinzani na pia akasisitiza kuwa hatakubali wawili hao waongoze wakazi kuingia upinzani.