Maoni

MAONI: Hukumu ya kifo dhidi ya Kabila itachochea moto vita Congo

Na DOUGLAS MUTUA October 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA barobaro aliyetembea nyuma ya baba yake, bunduki begani, kwa takriban kilomita 1,500 kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) hadi jijini Kinshasa na kupindua serikali, hukumu ya kifo ni mzaha wa mwaka!

Rais Mstaafu wa DRC Joseph Kabila Kabange, si mtu wa kutishiwa na hukumu sampuli hiyo, hasa ikiwa imetolewa na wanajeshi waliomwita amiri jeshi mkuu wao alipoiongoza nchi hiyo tangu 2001 hadi 2019.

Joseph hakurithishwa mamlaka na baba yake, Laurent-Desire Kabila, kama mwana wa kifalme, ila mzee wake huyo aliuawa kwa sababu za kisiasa akiwa ofisini, wakuu wa majeshi, wakubwa wake kazini hasa, wakaamua kumtawaza rais ili aiunganishe nchi akiwa na umri wa miaka 29 pekee.

Swali la iwapo Kabila mdogo alipiga hatua katika jaribio la kuiunganisha nchi au la halina jawabu moja kwa kuwa inategemea unayemuuliza.

Ukweli usiopingika ni kwamba, mpaka sasa ndiye mwanasiasa aliye na ushawishi mkubwa zaidi DRC.

Kwamba siku chache zilizopita mahakama ya kijeshi jijini Kinshasa imemhukumu kifo akiwa mafichoni, eti sasa ni mtoro wa kupigwa risasi kokote atakakopatikana ndani ya mipaka ya DRC, ni mzaha mkubwa unaoweza kusababisha kilio na maafa yasiyomithilika.

Serikali ya Rais Felix Tshisekedi inadai Bw Kabila ameingia ubia wa kisiasa na kundi la waasi la M-23, na ndiyo maana ameshtakiwa kwa baadhi ya makosa yanayoaminiwa kufanywa na waasi hao: uhaini, mauaji, ubakaji na kadhalika.

Mashtaka yaliendeshwa bila mshtakiwa mwenyewe kupandishwa kizimbani kwa kuwa anaishi nje ya nchi – mara nyingi Afrika Kusini – na wala hakuwa na mawakili, hivyo madai yalitolewa tu, yakakosa kupingwa, kesi ikaamuliwa.

Ingawa huenda Bw Kabila ana fursa ya kukata rufaa, ni vigumu kutabiri mchakato huo utakwenda vipi katika mazingira ambapo mfumo wa mahakama umedhibitiwa na kiongozi wa nchi.

Hukumu hiyo kali inanuiwa kutumiwa kama tishio kwa Bw Kabila ili aache kuwaunga mkono waasi wa M-23, na pia asiweze kuunganisha vyama vya upinzani ambavyo vinaweza kuiangusha serikali ya Rais Tshisekedi.

Waasi hao wanaitetemesha serikali si haba kwa kuwa wameshikilia maeneo mawili makuu ya mashariki ya DRC ambayo yamehodhi madini ya thamani kubwa. Walitwaa maeneo hayo kwa msaada wa majeshi ya Rwanda.

Asichoonekana kukijua Rais Tshisekedi ni kwamba, huenda hukumu hii ikaimarisha ukuruba wa Rais Paul Kagame wa Rwanda na Bw Kabila, washirika wa muda mrefu tangu enzi ya vita vilivyomng’oa mamlakani dikteta Mobutu Seseseko.

[email protected]