‘Shamba la Mkubwa’: Mamia wafurushwa makwao mwekezaji akitwaa ardhi Taveta
ZAIDI ya watu 300 wameachwa bila makao katika kijiji cha Mkocheni, Kaunti ya Taita Taveta, baada ya mwekezaji mmoja kuvunja nyumba zao usiku wa manane ili kupisha mradi mkubwa wa kilimo.
Kwa sasa mwekezaji huyo ameweka ua katika ardhi hiyo ya ekari 1,000 karibu na Ziwa Jipe.
Wenyeji wasema walifurushwa saa nane usiku wa kuamkia Jumapili na maafisa wa polisi waliokuwa wameandamana na maafisa wa utawala wa eneo hilo.
Ardhi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na aliyekuwa mbunge wa Taveta Basil Criticos, na mke wa Rais wa zamani, Mama Ngina Kenyatta.
Haijulikani jinsi mwekezaji mpya alikuja kuimiliki baadaye.
“Tuliamshwa kwa kishindo na kuambiwa tutoke nje mara moja. Hatukupewa muda wa kuokoa mali yetu,” alisema Bi Hamida Daudi, mmoja wa waathiriwa.
Bi Daudi asema wameishi hapo kwa vizazi vitatu na serikali ilikuwa imewaahidi kuwa watapewa hatimiliki.
Mnamo Juni, maskwota hao waliwasilisha kesi katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Voi dhidi ya Afisa wa Upimaji Ardhi Taveta, Waziri wa Ardhi na Mwanasheria Mkuu.
Mahakama ilitoa amri dhidi ya kuwafurusha hadi kesi hiyo isikilizwe na kukamilika.
“Hatujui ni nani huyu mwekezaji. Tunapouliza viongozi wetu, wanatuambia ‘Hili ni shamba la mkubwa’. Lakini huyu mkubwa ni nani ambaye hana utu?” alisema Bi Daudi.
Gavana wa Taita Taveta, Andrew Mwadime, alilaani vikali hatua hiyo akisema ni unyakuzi wa ardhi unaoendeshwa na watu wenye ushawishi serikalini.
Aliahidi kuchunguza suala hilo na kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka sheria za ardhi.
Kwingineko
Wakazi wa kisiwa cha Wasini wameapa kutoondoka katika ardhi ya ekari zaidi ya 600 ambayo hatimiliki yake ilikabidhiwa kwa familia ya Saggaf.
Mzee Fadhili Abdalla, 86, mmoja wa wakongwe zaidi katika kisiwa hicho alisema haiwezekani kwa familia moja kudai umiliki wa zaidi ya nusu ya kisiwa hicho.
“Jamii ya Wavumba imekaa hapa tangu miaka 500 iliyopita. Baada ya wakoloni kuja tuliteua familia hiyo kuwa mmoja wa wadhamini wa ardhi ya jamii, wala si mmiliki. Lakini sasa ametusaliti,” Bw Abdalla alisema.
Wakazi hao wanataka kuungana na kupinga uamuzi uliokabidhi hatimiliki kwa familia hiyo.
Bw Rashid Juma, mfanyibiashara wa kitalii kisiwani humo alisema hatua hiyo ni pigo kwa wenyeji waliowekeza kwenye sekta ya hoteli.
Katika ziara yake katika kisiwa hicho, Seneta Maalumu wa Kwale, Bw Raphael Chimera, aliahidi kuwasaidia wakazi hao kuwasilisha kesi katika mahakama ya rufaa ili kutetea ardhi hiyo.
Katika mahojiano ya awali, msemaji wa familia hiyo, Bw Muhammad Maula Saggaf, alisema walioekeza katika ardhi hiyo watalazimika kunua vipande hivyo ili kumiliki kisheria.
Pia aliomba serikali kununua kipande cha ardhi hiyo na kugawia maskwota, kwani familia haina nia ya kufurusha maskwota wanaoishi humo.