Kenya Moja sasa wamtaka Sifuna agombee urais, wamsihi Raila ampe baraka
VUGUVUGU la Kenya Moja, linaloongozwa na Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, limetangaza kuwa huenda likadhamini mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Hatua hii inaibua mtihani kwa mrengo wa serikali jumuishi na ule wa umoja wa upinzani.
Kundi hilo la kisiasa linaloshirikisha wanasiasa wenye umri mdogo limeonyesha dalili kwamba halitashirikiana na mirengo hiyo miwili kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Mrengo wa Serikali Jumuishi unaongozwa na Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga huku ule wa Umoja wa Upinzani unashirikisha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, Martha Karua wa chama cha People Liberation Party (PLP) miongoni mwa wengine.
Mnamo Jumapili, Mbunge wa Bumula, Jack Wamboka, alionyesha dalili kwamba kundi hilo liko tayari kumuunga mkono Bw Sifuna apambane na Rais Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.
“Tunaongea na ninavyomwona Seneta Sifuna na watu ambao tuko nao, ikifika 2027 hatutaogopa chochote. Ni heri tuwe na chaguo letu 2027,” Bw Wamboka akasema.
Kauli sawa na hiyo ilitolewa na Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi, aliyemsihi Bw Odinga awaachilie wafuate mkondo mwingine kisiasa kwa ajili ya kukomboa taifa hili.
“Utuachilie Baba (Raila) ili tuokoe nchi yetu kwa sababu tayari tumekupa takriban miaka 60 kutuongoza lakini hujaweza kuleta uthabiti nchini. Sasa utuachilie,” Bw Amisi akasema.
Mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Anthony Kibagendi, alisema Kenya Moja inayoshirikisha wabunge kutoka vyama mbalimbali, itahakikisha kuwa Rais Ruto na Bw Odinga wameshindwa uchaguzini.
Licha ya kwamba ndiye msemaji wa ODM, Bw Sifuna ameendelea kupinga Mkataba wa Maelewano (MoU) kati ya chama hicho na kile cha United Democratic Alliance (UDA) chake Rais Ruto.
Seneta huyo wa Nairobi ameelezea nia yake ya kugura ODM endapo itatangaza kumuunga mkono Rais katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Tangazo la hivi punde la Kenya Moja huenda likaathiri ODM endapo Bw Sifuna na wabunge wengine wa chama hicho watajiondoa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Vuguvugu hilo linashirikisha Bw Sifuna, Bw Amisi, Bw Kibagendi, Bw Wamboka, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Gathoni Wamuchomba (Githunguri), Clive Gisairo (Kitutu Masaba) na Mbunge wa Bomachoge Borabu Obadiah Barongo.
Huku wanasiasa hao wakidai serikali inalenga kuwagawanya, wameapa kushikana hadi watakapotwaa mamlaka mnamo 2027.
Tangazo la kundi hilo kwamba litadhamini mgombeaji urais linaashiria kuwa idadi ya wagombea urais inaongezeka kila uchao.
Hii ni licha ya kwamba tarehe ya uchaguzi mkuu ni Agosti 9, 2027, miaka miwili tu ijayo.
Ongezo la idadi ya wagombeaji urais pia linaongeza ushindani wa kiti hicho na kulingana na wadadisi hali hiyo huenda ikamfaidi Rais Ruto.