Ruto amwagia vijana Sh5 bilioni kujiendeleza kiuchumi kupitia mradi wa ‘Nyota’
SERIKALI inazidi kuanzisha mikakati mipya ya kiuchumi inayolenga kuwapa vijana fursa za kiuchumi huku uchaguzi mkuu wa 2027 ukikaribia.
Mkakati wa hivi punde ni uzinduzi wa mradi wa NYOTA unaolenga kuwapa vijana 100,000 pesa za kuanzisha biashara ndogondogo.
Jana serikali ilizundua mradi huo wa Sh5 bilioni katika hatua inayofasiriwa kama mbinu ya kuwashawishi vijana wamchague Rais William Ruto mnamo 2027. Kila kijana atapokea Sh50,000.
Katika utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa ushirikiano na serikali ya Kenya, amewatwika jukumu makatibu wake wote wa wizara washiriki vikao na vijana wa Gen-Z katika kaunti zote 47 nchini.
Vijana 70 kutoka kila wadi 1,450 kote nchini watanufaika na mpango huo. Mpango huo pia utawawezesha vijana 90,000 kupata mafunzo ya kazi.
Jana, waraka kutoka kwa Wizara ya Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogondogo ulionyesha kuwa makatibu walitumwa hadi kaunti zao za nyumbani kutoa hamasisho kwa vijana kuhusu mpango huo.
“William Ruto, Rais wa Kenya, ameamrisha makatibu wote kuelekea mashinani na kuhamisha vijana kuhusu mpango wa Nyota katika kaunti zote 47 kuanzia Jumatatu Oktoba 6,” wizara hiyo ikasema.
Rais aliwaamrisha makatibu waandae mikutano na magavana, wabunge, mabunge ya kaunti na machifu ili wahamasishwe kuhusu mpango huo.
Wakati wa mkutano katika Ikulu na makatibu hao, Rais Ruto alisema Nyota ni mradi utakaopanua nafasi za ajira kwa vijana.
Alisema kuwa pamoja na ujenzi wa nyumba za bei nafuu, kazi za mitandao, vibarua mpango huo wa Nyota utawasaidia vijana kuwa wavumbuzi na wafanyabiashara mahiri.
Katibu wa Biashara Ndogo-ndogo Susan Mang’eni ambaye mradi huo uko chini ya wizara yake, alisema lengo kuu ni kuimarisha maisha ya vijana ili wajitegemee kimapato.
“Mradi huu unalenga kubuni ajira, kuongeza nafasi za kazi, kuwawezesha vijana kuweka akiba na kuwasaidia kupata masoko ya kuuza bidhaa zao,” akasema Bi Mang’eni.
Kulingana na waraka kwa makatibu, Fikirini Jacobs ambaye ni Katibu wa Masuala ya Vijana, alikuwa katika Ukumbi wa St Thomas Kilifi, naye Idris Dokata (Masuala ya Baraza la Mawaziri) akivumisha Nyota katika Shule ya Msingi ya Hola huku Mohamed Dahar (Uchukuzi) akiwa katika ukumbi wa Ronald Ngala, Mombasa.
Katibu wa Biashara, Abubakar Hassan alikuwa Lamu, Shadrack Mwadime (Leba) akiwa ukumbi wa Mwatate naye Aden Milaa (Uchukuzi wa Majini) akiwa Chuo Kikuu cha Garissa.
Mohamed Bashiri (Teknolojia) alikuwa Wajir huku Ahmed Abdisalam akivumisha mpango huo Mandera.
Rais Ruto aliingia madarakani mnamo 2022 kwa ahadi ya kubuni nafasi kadhaa za ajira kwa vijana akiwapa kipaumbele wale wa mapato ya chini na akaahidi kushusha gharama ya maisha.
Pia aliziegemeza kampeni zake katika kuwainua vijana huku akikashifu viongozi wa wakati huo kwa kuchangia taifa kutopiga hatua kimaendeleo.
Hata hivyo, nyingi ya ahadi hizo hazikutekelezwa ndiposa Gen-Z wakajibwaga barabarani mwaka jana na mwaka huu kulalamikia uchumi mgumu na dhuluma za serikali.
Kuelekea uchaguzi wa 2027, Rais Ruto na upinzani wote wanamakinika kuhakikisha kuwa wanapata kura za vijana.
Wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Madaraka Kaunti ya Homa Bay, Rais alisema mpango huo wa Nyota unalenga kuwapiga jeki vijana 800,000 ambao wako kati ya umri wa miaka 18-29 na waliofika umri wa miaka 35 na walemavu.
Mbali na Nyota, Rais na viongozi katika utawala wa sasa wamekuwa wakishiriki michango ya kuyainua makundi ya wahudumu wa bodaboda, mama-mboga huku wakisisitiza kuwa utawala wa sasa umebadilisha nchi kiuchumi.