Makala

Mbunge atoa kauli ya kuashiria Raila anatibiwa ng’ambo

Na KASSIM ADINASI October 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RIPOTI zinazokinzana zinaendelea kuenea kuhusu hali ya afya ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga huku Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi akitoa kauli zinazofasiriwa kuwa Waziri huyo Mkuu wa zamani anaugua.  

Bw Omondi Jumapili aliwataka Wakristo kote nchini Kenya kufanya maombi maalum ili Bw Odinga apone. Hii ni licha ya kwamba Afisi Kuu ya Raila ilikuwa imekanusha kuwa Kinara huyo wa ODM anaugua.

Sekretariati hiyo ilisema Bw Odinga aliondoka nchini Ijumaa kuenda safari zake za kawaida ng’ambo wala hakuwa Ulaya jinsi ambavyo baadhi ya mabloga na taarifa za mitandao zilivyoashiria.

Akizungumza wakati wa Harambee katika eneo la Rang’ala, Kaunti ya Siaya, ambako alikuwa mgeni wa heshima, Bw Omondi, ambaye aliwahi kuwa msaidizi wa kibinafsi wa Raila, alitoa wito wa umoja wa kitaifa kupitia maombi.

“Natoa wito kwa Wakristo wote wa madhehebu yote kote nchini Kenya kufanya maombi maalum kwa ajili ya kiongozi wetu, Raila Odinga, ili apate afueni ya haraka na kurejelea afya njema na nguvu zake. Anapopumzika hospitalini, tunamkumbuka sana katika mawazo na maombi yetu,” akasema Bw Omondi.

Afisa mwingine wa ODM aliyefichua taarifa kwa Taifa Leo kwa masharti ya kutotajwa jina alisema Bw Odinga alisafiri kwa uchunguzi wa kawaida wa kiafya.

 Afisa huyo alikataa kutoa maelezo zaidi kuhusu hospitali anakopewa matibabu Bw Odinga.

 Aidha, afisa huyo alieleza kuwa Bw Odinga amekuwa akichunguzwa kiafya mara kwa mara tangu upasuaji wa kichwa aliofanyiwa mwaka 2010.

Raila alifanyiwa upasuaji wa kichwa Juni 2010 ili kupunguza shinikizo lililokuwa limejitokeza nje ya ubongo wake, huenda kutokana na kugonga kichwa chake kwenye gari.

Madai ya kuugua kwa Bw Odinga yaliibuka baada yake kupunguza shughuli nyingi za umma, ikiwemo matukio makubwa ya kisiasa ya chama chake cha ODM, hali iliyochochea uvumi kuhusu afya yake.

Alikosekana katika mikutano ya kisiasa ya chama hicho iliyofanyika katika kaunti za Kisii, Wajir na Narok katika maandalizi ya sherehe za kuadhimisha miaka 20 ya chama hicho kitaifa.

Hata hivyo, Bw Odinga alionekana hadharani baada ya kuongoza kikao cha mashauriano cha chama hicho kuhusu maandalizi ya sherehe hizo katika Hoteli ya Serena jijini Nairobi mnamo Oktoba 3.

Hali ya afya ya Bw Odinga imekuwa mada ya umma na vyombo vya habari katika siku za hivi majuzi, jambo lililomlazimu msemaji wake na wafuasi wake kujibu madai hayo kwa kulaumu wapinzani wa kisiasa kwa kuzusha uvumi huo.

Naibu Rais wa zamani, Rigathi Gachagua, ambaye ODM imemtuhumu kuwa miongoni mwa walioeneza uvumi huo, siku ya Jumapili alisema Bw Odinga anapaswa kujitokeza hadharani kuonyesha kuwa yuko salama badala ya kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.

“Ikiwa kiongozi anasemekana kuwa mgonjwa, na yeye yuko salama, anatakiwa tu kupuuza na kuendelea na shughuli zake. Lakini kama uvumi huo unamkera na anataka kuonyesha kuwa yuko salama, hahitaji kuandika barua. Kinachohitajika ni kushiriki tu shughuli chache za umma, na watu wataona kuwa yuko vizuri, na uvumi utakwisha,” alisema Bw Gachagua katika mahojiano na runinga ya KTN.

“Rais Moi alikuwa akifanya hivyo. Angepotea kwa siku tano au sita, watu wangesema ni mgonjwa. Kisha angejitokeza katika jumba la KICC, atembee kwa kasi kutoka KICC hadi Harambee House, na mjadala ungeisha papo hapo.”

Mjadala kuhusu afya ya Bw Odinga pia uliibuka kuwa mada kuu katika tamasha la kitamaduni la Sigand Nyi Nam (Hadithi za Mabinti wa Ziwa) lililofanyika katika uwanja wa Jaramogi Oginga Odinga.

Katika hafla hiyo, viongozi wa kike walionyesha hasira zao kuhusu kile walichokiita kampeni ya makusudi ya kupotosha umma kuhusu hali ya afya ya Bw Odinga.

Mbunge wa Kisumu Magharibi, Rosa Buyu, alikanusha madai hayo na kumkosoa vikali Bw Gachagua.

“Kuna huyu mtu, Gachagua anayefikiri kuwa njia pekee ya kuongoza ni kwa kumchafulia jina Raila Odinga. Mtu amkumbushe kwamba afya ya Raila si jambo linalomhusu. Hata kama Raila angekuwa mgonjwa, nia mbaya zake hazitafanikiwa,” alichemka kwa ukali.

Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga, pia alikosoa matamshi ya Bw Gachagua akisema yanadhihirisha mtazamo finyu wa kisiasa.

“Tunahitaji kiongozi anayezungumza kwa niaba ya taifa zima, si yule anayeamka kila asubuhi akifikiria Mlima Kenya pekee,” akasema Bi Wanga.

Aliwaomba viongozi wengine wa upinzani kuwa waangalifu wanapochukua msimamo wa kisiasa wa BwGachagua, akionya kuwa matamshi yake ya kugawanya taifa yanaweza kuhatarisha umoja wa kitaifa.