Habari za Kitaifa

Mwanariadha mkongwe Hezekiah Nyamau aliyeletea Kenya fahari aaga dunia

Na WYCLIFFE NYABERI October 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANARIADHA mkongwe Hezekiah Nyamau ameaga dunia. 

Nyamau, 88, alifariki Jumanne asubuhi katika hospitali moja jijini Nakuru kulingana na mjukuu wake Felister Nyamau.

“Mzee alipumzika leo asubuhi mwendo wa saa nane asubuhi katika hospitali moja mjini Nakuru. Mapenzi ya Bwana yametimia,” Bi Nyamau aliambia Taifa Spoti kwa simu.

Mwanariadha huyo wa zamani amekuwa hospitalini kwa Mudavadi akipambana na saratani ya kibofu cha mkojo.

Nyamau alikuwa miongoni mwa wanariadha wanne walioishindia Kenya medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki ya Munich ya 1972 pamoja na Charles Asati, Julius Sang na Robert Ouko.

Kifo cha Nyamausasa kinamwacha Bw Asati kuwa mwanariadha pekee aliyesalia kutoka kwa kikundi cha wanne hao walioiletea Kenya heshima na hadhi.

Alipokuwa amelazwa hospitalini, Nyamau aliilia serikali kwa kile alichosema ni kumtelekeza, na kuiachia familia yake mzigo wa kubeba bili za hospitali peke yao.

Kabla ya kuhamishwa hadi Nakuru kwa matibabu maalum, Nyamau alikuwa katika kituo kingine katika Mji wa Kisii.

Akiwa Kisii, aliomba Wakenya wenye nia kumfaa.

“Wanangu, kama mnavyoona, sina nguvu ya kuzungumza. Piga picha zangu tu na mwonyeshe nchi aliko mwanariadha aliyeiletea Kenya heshima. Wale wanaoweza kunisaidia na wafanye hivyo,” Nyamau alitamka maneno hayo ya kuatua moyo.

Aligundulika kuwa na saratani Februari mwaka huu kulingana na mtoto wake mzawa wa pili, Pamela.

Nyamau alizaliwa na kukulia katika kijiji cha Nyaguta, eneo bunge la Nyaribari Chache kaunti ya Kisii. Kando na medali ya dhahabu ya Olimpiki ya 1972, pia alishinda fedha katika hafla hiyo hiyo kwenye michezo ya 1988 huko Mexico pamoja na wengine.

Kwa sababu ya umahiri wake katika riadha, Nyamau alijiunga na jeshi la Kenya mwaka wa 1963 na kustaafu mwaka wa 1997.

Licha ya kuwa mmoja wa wanariadha wa Kenya walioenziwa, maisha yake hayakuwa sawa tangu kuondoka kwake jeshini.

Katika mahojiano na runinga ya NTV mwaka mmoja uliopita, Nyamau alisimulia jinsi ilivyokuwa vigumu kwake kujikimu kwani alikuwa ametumia akiba yake yote kuwasomesha watoto na wajukuu wake.

Mwanariadha huyo nguli alisema licha ya kuwapa elimu, wengi wao walisalia bila ajira na kuhangaika kutafuta riziki, jambo ambalo alisema lilikuwa likitatiza ustawi wake zaidi.

Nyamau pia aliikashifu serikali na kuishutumu kwa kutojituma kuboresha ustawi wa wanariadha wanaozeeka ambao waliiletea Kenya fahari katika majukwaa ya kimataifa.

“Serikali inaonekana imetupuuza licha ya kuleta heshima nchini. Ukienda kwa wanariadha wengi wa enzi zetu, utasikitikia hali yao. Tunahitaji kutambuliwa kwa kuiwakilisha Kenya vyema katika nyanja za kimataifa na ustawi wetu unapaswa kuboreshwa,” Bw Nyamau alilalamika.