Habari za Kaunti

Mzozo wa ardhi Taveta wazidi chifu akidai kutishiwa maisha

Na LUCY MKANYIKA October 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Chifu wa eneo la Jipe lililo katika Kaunti Ndogo ya Taveta, Taita Taveta, amedai kuwa maisha yake yamo hatarini baada ya kushambuliwa na maafisa wa GSU waliokuwa wakiwaondoa wakazi kutoka kwa shamba lenye utata la ekari 1,000.

Bw Sharia Bwire alisema alishambuliwa Jumatatu asubuhi alipokuwa akisubiri chifu wake ili waende kwenye kikao walichokuwa wamepanga.

“Nilikuwa njiani kuelekea afisi ya chifu na nilipofika kwa lango la shamba hilo nikamkuta Naibu Kamishna wa eneo hili akihutubia maskwota waliokuwa wameondolewa. Hakuwa amenijulisha kuwa angekuja katika eneo langu,” alisema.

Bw Bwire alisema alimsalimu Naibu Kamishna Chaka Nyamawi, ambaye alimjibu lakini akaendelea kuhutubia umati. Baadaye, maafisa wa GSU walimkaribia Bw Bwire na kumtaka ajitambulishe.

“Nilijitambulisha kuwa mimi ni naibu chifu wa eneo hilo, wakaniacha,” alisema.

Hata hivyo, baada ya DCC kuondoka, naibu chifu huyo alibaki akisubiri chifu wake lakini alipokuwa anangoja, afisa mmoja wa GSU alianza kumpiga.

“Alidai ana taarifa kuwa nilichochea maskwota hao wasiondoke. Alinipiga teke na kunikanyaga hadi wenzake wakaja kumzuia,” alieleza.

Alidai kuwa, afisa huyo alimtishia maisha na kumuonya dhidi ya kukaribia eneo hilo.

“Alisema atanimaliza. Nilimuuliza kosa langu ni nini, lakini akasema hataki kuniona pale. Nikamwambia anipige risasi kama anataka,” alisema.

Baada ya maafisa wenzake kumzuia, afisa huyo alimpigia simu Bw Nyamawi ambaye alirudi lakini, kwa mujibu wa Bwire, hakumsikiliza bali alichukua picha zake na pikipiki yake, akamtishia kumchukulia hatua.

Juhudi za kumhoji Bw Nyamawi kuhusu suala hilo hazikufua dafu, kwani awali alisema alikuwa mkutanoni ila baadaye hakupatikana.

Bw Bwire alisema kuwa tangu zoezi hilo la kuwahamisha maskwota hao lianze, amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa wakubwa wake.

Aliongeza kuwa, aliwahi kuitwa na maafisa wa upelelezi kuhusu madai ya kupanga kushambulia maskwota kwa moto. Hata hivyo, alisema madai hayo yalikuwa ya uongo.

“Niliwaambia waite wale waliokuwa wana madai hayo ili nijue kama ni ya kweli. Hadi leo hakuna ushahidi wowote umepatikana,” alieleza.

Baada ya kushambuliwa mnamo Jumatatu, aliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi cha Taveta na kupata matibabu katika hospitali ya kaunti ndogo ya Taveta.

Wakati huo huo, serikali ya Kaunti ya Taita Taveta imelaani vikali zoezi hilo la kuwaondoa wakazi, ikilitaja kuwa kinyume cha sheria, la kikatili na linalokiuka haki za binadamu.

Katika taarifa rasmi, kaunti hiyo ilisema kuwa zoezi hilo lilifanyika kinyume na amri ya mahakama ya Juni 25, 2025.

“Matumizi ya polisi bila kibali cha mahakama ni uvunjaji wa sheria. Ardhi ya watu wa Taita Taveta haitachukuliwa kwa nguvu,” ilisoma sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na msemaji wa serikali hiyo Bi Mchikirwa Ndelejai.