Habari

Raila ni buheri wa afya, Ida asema

Na George Odiwuor October 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

FAMILIA ya kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, hatimaye imezungumza hadharani kufuatia uvumi ulioenea kwa siku kadhaa kuhusu hali ya afya ya Waziri Mkuu huyo wa zamani.

Mkewe, Bi Ida Odinga, amewahakikishia Wakenya kuwa mumewe yuko katika hali nzuri na hana tatizo lolote la kiafya.

Akizungumza kwa mara ya kwanza hadharani tangu uvumi huo uanze, Bi Ida alikiri kuwa amefahamu kuhusu madai ya hali ya afya ya mumewe. Alisema uvumi huo umezusha hofu miongoni mwa Wakenya wengi.

“Kuna watu wanaosema Baba ni mgonjwa. Lakini nataka niseme wazi kuwa, hana ugonjwa wowote,” alisisitiza.

Kukosekana kwa Raila katika shughuli za hadhara kumeibua tetesi kwamba huenda alisafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Jumapili iliyopita, Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi, ambaye aliwahi kuwa msaidizi wa karibu wa Raila, aliwaomba Wakenya kumuombea kiongozi huyo.

“Naomba Wakristo wote, kutoka kila dhehebu nchini Kenya, wamuombee kiongozi wetu Raila Odinga ili apate nafuu kamili. Tunamuombea kwa moyo wa dhati,” alisema wakati wa mchango wa fedha katika kaunti ya Siaya.

Kauli hii ilipingana na msimamo wa msemaji wa Raila, Bw Dennis Onyango, ambaye amekuwa akisisitiza kuwa Raila si mgonjwa, akieleza kuwa uvumi huo unasambazwa na wapinzani wa kisiasa.

Bi Ida aliendeleza msimamo huo alipohudhuria uzinduzi wa Mpango wa Matibabu ya Fistula katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Migori, alikoaliwa na Gavana Ochilo Ayacko.

“Kama hali yake ingekuwa mbaya hivyo, ningemleta hapa Migori atibiwe. Baba yuko salama, na anawasalimu. Amechukua mapumziko mafupi tu,” alisema.

Alisisitiza kuwa mumewe yuko katika mapumziko mafupi kutoka kwa shughuli za umma, na si mgonjwa kama inavyodaiwa.

“Mimi naishi naye, najua hali yake ya afya kuliko mtu mwingine yeyote. Inakuwaje mtu asiyeishi naye anajua hali yake kuliko mimi? Nimewaambia ukweli,” alisema Ida.