Mbunge akemea ongezeko la unyakuzi wa ardhi ya viwanja vya michezo mashinani
MBUNGE wa Shinyalu, Fred Ikana ameeleza wasiwasi kuhusu hali mbaya ya viwanja vya michezo vya umma na wizi wa ardhi pamoja na ujenzi usiofuata sheria katika eneo hilo la uwakilishi bungeni.
Ikana alitoa ujumbe huo siku chache tu baada ya kudhamini mashindano ya FKF Mini-League katika jimbo hilo lake.
Mbunge huyo alielezea mipango kabambe ya kukuza talanta miongoni mwa vijana wa eneo hilo, huku akitoa wito kwa Serikali ya Kaunti ya Kakamega ihifadhi na kulinda vifaa vya michezo vya umma.
“Kakamega ni nyumbani kwa wanaspoti wengi. Ni kaunti iliyo na historia kubwa ya kukuza vipaji katika taaluma mbalimbali za michezo, ikiwemo soka, riadha, raga, na mpira wa wavu,” alisema Ikana ambaye alishirikiana na Shirikisho la Soka Nchini (FKF) kudhamini mashindano ya Ligi Ndogo ya Jimbo la Shinyalu kati ya Septemba 28 na 29.
“Afya ya vijana ni muhimu kwa ustawi wao wa sasa na wa baadaye. Kipindi cha miaka ya utineja huambatana na mabadiliko makubwa ya mwili, kihisia na jamii, ambayo yanaweza kuwa na athari kubwa kwenye afya na tabia zao kwa maisha yao yote,” aliongeza.
Wakati wa Ligi Ndogo, Mugomari iliibuka mshindi baada ya kushinda Samba Ileho 3-1.
Washindi walifuzu kwa fainali hiyo baada ya kushinda Shipalo Giants 1 (5)- 1 (4) katika nusu fainali. Simba Ileho iliizima Shipalo Corinthians 1-0 kwenye nusu fainali nyingine.
Aliahidi kumfikia Waziri wa Michezo na Masuala ya Vijana, Salim Mvurya kumkumbusha kuhusu ujenzi wa kituo cha kukuza vipaji katika Shule ya Upili ya Shanderema.
“Tunahitaji akademia za michezo kote Kakamega ili vijana wapate fursa ya kukuza vipawa vyao kupitia michezo mbali mbali kuanzia ngazi ya chini,” alisema.
Ikana ambaye majuzi alizuri Amerika na kukutana na wasimamizi wa Visual Soccer Academy eneo la Iowa alizawadi timu nne zilizoshiriki katika nusu fainali ya Ligi Ndogo ya Shinyalu.