Handisheki nyingine? Ruto na Gideon wakutana faraghani Ikulu
RAIS William Ruto na Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi, Jumatano, Oktoba 8, 2025 walikutana kwa mazungumzo ya faragha katika Ikulu ya Nairobi katika kile kinachotajwa kama jitihada za Rais kumshawishi Moi kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha useneta kaunti ya Baringo kufuatia kifo cha Seneta William Cheptumo.
Mkutano huo usiotarajiwa, ambao umeibua minong’ono ya maridhiano ya kisiasa kati ya wawili hao waliokuwa wapinzani wakuu katika siasa za Rift Valley, ulihusu zaidi uchaguzi mdogo wa Novemba 27.
Kulingana na vyanzo vya ndani ya Kanu, Rais Ruto alimtaka Moi kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho ili kumpa nafasi mgombea wa UDA, Vincent Chemitei.
Hata hivyo, Bw Moi alikataa pendekezo hilo licha ya ombi la moja kwa moja kutoka kwa Rais mwenyewe.
“Rais alitoa ombi hilo kwa heshima kubwa, lakini Mwenyekiti alikataa kwa ustaarabu,” alisema afisa mmoja wa Kanu.
Hata hivyo, maafisa wa Ikulu waliozungumza kwa masharti ya kutotajwa majina walisema Moi alikubali kujiondoa ila akaomba muda wa kuzungumza na viongozi wa chama kabla ya kutoa tangazo rasmi.
“Amekubali kujiondoa katika uchaguzi wa Baringo,” alisema afisa wa Ikulu.
Moi aliandamana na Katibu Mkuu wa Kanu George Wainaina na aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake Baringo, Gladwell Cheruiyot.
Inasemekana kuwa biashara ya familia ya Moi, ambayo imeshuhudia changamoto nyingi chini ya utawala wa Rais Ruto, pia ilikuwa sehemu ya mazungumzo.
Hii inaashiria kuwa mazungumzo hayo hayakuwa tu ya kisiasa, bali pia ya kiuchumi kwa lengo la kutafuta njia ya maelewano ya muda mrefu kati ya pande hizo mbili.
Wachambuzi wa siasa wanasema Rais Ruto ana hofu ya aibu endapo UDA itapoteza kiti hicho ambacho kiko ngome yake.
Baringo imekuwa ikizingatiwa kama ngome ya kisiasa ya Rais tangu 2022 alipompokonya Moi karibu viti vyote vya ubunge na MCA katika eneo hilo.
“Kushinda Baringo kutampa nguvu Moi na wapinzani wengine kuhoji uwezo wa Ruto kudhibiti ngome yake,” alisema mchambuzi wa siasa Dismas Mokua.
Katika uchaguzi wa 2022 William Cheptumo (UDA) alipata kura 141,177, Gideon Moi (Kanu) alipata kura 71,480 na mgombea huru Felix Chelaite alipata kura 3,261.
Kwa mujibu wa maafisa wa Kanu, Moi anaona huu ni wakati muafaka wa kufufua Kanu na kurejesha heshima ya familia ya Moi katika siasa za kitaifa, hasa katika eneo la Rift Valley.
“Mwenyekiti anahisi ni wakati wa kujenga upya Kanu kutoka mashinani,” alisema afisa mmoja wa Kanu.