Mdosi mkaidi: Katibu asusia mialiko ya Wabunge mara 16!
KATIBU wa Wizara ya Fedha, Chris Kiptoo, anakumbwa na presha kali kutoka kwa Wabunge kwa kukosa vikao vya kamati ya Bunge mara 16 ambapo alitarajiwa kutoa maelezo kuhusu matumizi ya fedha za umma.
Kamati ya Bunge ya Hesabu Maalumu imeonyesha ghadhabu kubwa dhidi ya Dkt Kiptoo kwa kukosa kufika mbele yake na kutoa maelezo kuhusu mabilioni ya fedha zilizotengewa taasisi 14 zilizo chini ya usimamizi wake.
Tangu mwaliko wa kwanza mnamo 2023 hadi mwaliko wa hivi karibuni zaidi Jumatano, Oktoba 8, 2025, Katibu Kiptoo hajawahi kupata muda wa kufika mbele ya kamati hiyo inayosimamiwa na Mbunge wa Migori, Fatuma Mohamed.
Katika taarifa yenye ujumbe mzito, kamati hiyo imemtaja Dkt Kiptoo kama kikwazo katika utekelezaji wa jukumu lao la kuchunguza matumizi ya fedha za umma zilizotengewa hazina mbalimbali chini ya mamlaka yake.
“Kikwazo kikubwa ni kuendelea kukosa kufika mbele ya Kamati, licha ya kualikwa mara kwa mara. Ukosefu huu wa ushirikiano umeathiri maendeleo ya uchunguzi na kuzuia utekelezaji wa jukumu la katiba la kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilmali za umma,” ilisema taarifa ya kamati baada ya katibu huyo kukosa kutii mwaliko tena.
Kamati imesema hadi sasa imemaliza uchunguzi wa hazina 50, huku 14 chini ya Katibu Kiptoo zikiwa bado na maswali anayopaswa kujibu.
Kuhusu hazina hizo 14, kumalizika kwa uchunguzi kutakuwa hatua kubwa katika kuondoa mzigo wa kazi na kuimarisha uwajibikaji katika usimamizi wa hazina maalumu.
Kamati hii, iliyoanzishwa chini ya Kanuni ya Kudumu namba 205, ni mojawapo ya kamati sita za Bunge zinazolinda maslahi ya umma, zinazohusika na kuchunguza ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kuhusu hazina zilizoanzishwa kwa sheria au kwa kanuni ndogo.
Ripoti za hazina hizo 14 zinahusiana na miaka ya kifedha 2017/2018 hadi 2023/2024.
Hazina hizo 14 ni sehemu kubwa ya zinazozingatiwa na Kamati ya Hesabu Maalum, zikiwemo Hazina ya Vijana Vijijini, Hazina ya Mikopo ya Mitaa, Hazina ya Usawa, Hazina ya Michango ya Umoja wa Afrika na Taasisi Nyingine za Kimataifa, Hazina ya Hifadhi ya Jamii.
Pia kuna Hazina ya Dharura, Hazina ya Kodi ya Maendeleo ya Mafuta, Hazina ya Kushughulikia Dharura ya Covid-19, na Mpango wa Dhamana ya Mikopo.
Katika barua aliyotumia Katibu wa Bunge, Samuel Njoroge, Dkt Kiptoo alisema alikuwa Washington DC, Amerika, akihudhuria mkutano wa mwaka wa Benki ya Dunia na Shirika Fedha la Kimataifa (IMF), hivyo hakuweza kuhudhuria kikao cha kamati hiyo.
Barua hiyo ya Oktoba 3, 2025, ilihusu kukosa kuhudhuria kikao cha Oktoba 7 pekee na si zile 15 zilizotangulia.
Taifa Leo ilijaribu kumpigia simu na kumtumia ujumbe mfupi Dkt Kiptoo kuelezea sababu za kukosa vikao vingine lakini hakujibu.
Ibara ya 125 ya Katiba inapatia Bunge mamlaka ya kuagiza mtu yeyote kutoa ushahidi au taarifa mbele yake.
Aidha, sheria ya Mamlaka na Haki za Bunge inapatia kamati za Bunge uwezo wa kulazimisha mashahidi kuhudhuria na kutoa ushahidi chini ya kiapo.