Habari za Kitaifa

Shahidi akiri kuwa mwizi kabla kuingia kanisa la Mackenzie

Na BRIAN OCHARO October 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHAHIDI katika kesi ya mauaji ya Shakahola alishangaza mahakama alipofichua kwamba alikuwa akipora Wizara ya Fedha alikofanya kazi kabla kujiuzulu alipojiunga na kanisa la mhubiri Paul Mackenzie.

Bi Vivian Malegua alisimulia jinsi aliacha kazi yake ya uhasibu katika ofisi za wizara hiyo tawi la Voi ili “aache kutenda dhambi”.

Kulingana naye alikuwa mwizi hadi pale Mackenzie alihubiri kuwa kuna kazi huelekeza watu katika dhambi.

“Kama mhasibu nilikuwa nimegeuka mwizi. Niliamua kujiuzulu kwa sababu Yesu hawezi kunipa kazi itakayofanya niwe mwizi. Kwa sasa nafanya biashara ndogo ndogo na vibarua,” aliambia mahakama chini ya uongozi wa Naibu Mkurugenzi Mwandamizi wa Mashtaka ya Umma, Jami Yamina.

Bi Malegua alisema mara ya kwanza kusikia kuhusu kanisa la Good News International (GNI) alikuwa ameenda kutembelea ndugu zake Malindi, akajiunga na kanisa hilo bila kushawishiwa na mtu yeyote.

Alifichua jinsi waumini walifundishwa kwamba elimu, tiba, na mapambo ya urembo ni kinyume na mafundisho ya Yesu Kristo, na kwamba bado anaamini katika baadhi ya mafundisho hayo.

“Nilihudhuria semina kadhaa. Tuliambiwa kwamba kanisa lilikuwa linaenda jangwani, kumaanisha hatungehudhuria tena makanisa ya kawaida,” alieleza.

Alisimulia pia jinsi alimtembelea rafiki yake, Bi Everlyn Mwangoji, ambaye alikuwa amehamia Shakahola na watoto wake watano wenye umri wa miaka kati ya mitano na 12.

Mara yake ya mwisho kuwasiliana na Mwangoji ilikuwa Aprili 2023, muda mfupi baada ya habari za mauaji ya Shakahola kuripotiwa.

“Kama wote walikufa, ningependa kujua kilichowapata,” alisema.

Wakati wa kuhojiwa na wakili wa Mackenzie, Bw Lawrence Obonyo, alisisitiza kuwa imani yake ni hatua ya kibinafsi.

Alikiri kuwa wengi ambao hawakukubaliana na mafundisho ya Mackenzie waliondoka kanisani. Hivi majuzi, shahidi mwingine pia alisema alikuwa mwizi wa bunduki kabla kujiunga na kanisa la Mackenzie.

“Hiyo ilikuwa zamani. Nilirekebisha tabia kabla kujiunga na kanisa,” alisema shahidi huyo.

Wakati huo huo, raia wa Tanzania alieleza mahakama jinsi mafunzo ya Mackenzie yalivunja familia yake.

Bw Ernest Vedasto Mwombeki, raia wa Tanzania, alidai Mackenzie ndiye alimsaidia mke wake kutoroka hadi Mbeya, Tanzania, kisha hadi msitu wa Shakahola, ambako alipotea pamoja na watoto wao watatu.

Mkewe, Bi Judith Assery Mwandary, alikimbia nyumbani kwao Arusha mnamo Februari 28, 2022, akiwa na watoto wao watatu wa kiume wenye umri wa miaka kati ya miwili na 10.

Bw Mwombeki aliripoti kutoweka kwao shuleni na kwa polisi siku iliyofuata na kuanza kuwatafuta bila mafanikio.

Mnamo Agosti 25, 2022, mkewe aliwasiliana naye kupitia nambari ya Kenya akiomba pesa za chakula.

Alimtumia, na tangu wakati huo aliendelea kuomba pesa za matumizi na nauli, akisema alitaka kurudi nyumbani baada ya kufichua kwamba alikuwa Kilifi.

Aliendelea kumtumia pesa, lakini hakurudi licha ya maombi yake.

Mnamo Januari 31, 2023, walizungumza tena, na pia akazungumza na watoto. Siku mbili baadaye, alimuomba pesa zaidi za kununua sabuni na maji ili kujiandaa kwa safari ya kurudi nyumbani, na alimtumia.

Siku hiyo, Bi Mwandary alimpigia tena simu akisema alikamatwa na polisi kwa deni alilokuwa akidaiwa na wanawake wa kikundi cha akiba.

Alimuomba msaada, naye akalipa deni hilo la Sh3,300 kupitia nambari ya Samuel Ocheya.

Walizungumza mara ya mwisho Februari 4, 2023, na baadaye Bw Mwombeki alisafiri hadi Kilifi kuwatafuta ambapo alishauriwa kuelekea Chakama ambapo waumini wa kanisa la Mackenzie walikuwa wakiishi.

Alielezwa mkewe na watoto waliwahi kuonekana hapo lakini wakati huo hawakuwepo, na hadi sasa hawajulikani waliko.