Habari

Kanjo aliyejirusha kutoka orofa ya 6 ‘alihusika na hongo’

Na NDUBI MOTURI October 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

AFISA mmoja wa usalama wa Kaunti ya Nairobi aliyefariki baada ya kujirusha kutoka orofa ya sita ya jengo la City Hall Annex mwezi Mei 2025, hakuwa kazini siku hiyo.

Alikuwa akichunguzwa kwa madai ya kuitisha hongo, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyowasilishwa katika Kamati ya Sheria na Haki ya Bunge la Kaunti ya Nairobi (JLAC).

Afisa huyo, Oscar Mungai Kanyi, alikuwa kwenye likizo rasmi na alitarajiwa kuripoti kazini Juni 10, 2025.

Hata hivyo, mnamo Mei 31, alionekana akiwa amevalia sare rasmi za Kaunti karibu na jengo la Nation Centre katika Barabara ya Kimathi — eneo ambalo limekuwa likipigwa darubini kwa visa vya unyanyasaji vinavyofanywa na maafisa wa Kaunti.

Kulingana na taarifa zilizowasilishwa mbele ya kamati inayoongozwa na MCA wa Mugumoini, Jared Akama, marehemu Mungai alionekana akiwa na raia mmoja aitwaye Joseph Muchiri ikidaiwa walikuwa wakiitisha hongo kutoka kwa madereva.