Habari za Kitaifa

KNH yalemewa na wagonjwa migomo ikiendelea Nairobi, Kiambu

Na MERCY CHELANGAT October 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HOSPITALI ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) imejipata katika hali ngumu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wanaofika kwa wingi, hasa kutoka kaunti za Nairobi na Kiambu, ambapo huduma nyingi za afya zimelemazwa na migomo inayoendelea.

Katika taarifa rasmi, Afisa Mkuu Mtendaji wa KNH, Dkt Richard Lesiyampe, alisema hospitali hiyo sasa imekuwa kituo kikuu cha kutibu wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura, huku hospitali nyingi za kaunti zikikosa kufanya kazi kikamilifu kutokana na migomo ya wahudumu wa afya.

“Hali hii imesababisha ongezeko kubwa la wagonjwa mahututi wanaofikishwa hapa, wengi wao wakiwa katika hali mbaya. Kwa masikitiko, baadhi ya kina mama na watoto wamekuwa wakifika hospitalini wakiwa wamechelewa sana, hali iliyosababisha vifo au matokeo mabaya ya kiafya licha ya juhudi kubwa za madaktari wetu,” akasema.

Aliongeza kuwa mahitaji ya huduma yamekuwa makubwa mno, jambo ambalo limeongeza shinikizo kwa huduma muhimu kama vyumba vya upasuaji, hifadhi ya damu na vipimo vya uchunguzi.

“Wafanyakazi wetu wanafanya kazi usiku na mchana, lakini rasilimali zetu zimepungua mno,” aliongeza.

Dkt Lesiyampe alitoa wito kwa wahusika wote kutatua tofauti zao kwa haraka, akisema kurejeshwa kwa huduma za kawaida katika hospitali za Kaunti ya Nairobi na Kiambu kutasaidia kupunguza shinikizo kwa KNH na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma kwa wakati katika maeneo yao.

Kiambu, madaktari wamekuwa katika mgomo tangu Mei 27, 2025, wakilalamikia kucheleweshwa kwa mishahara, ukosefu wa bima ya afya, kutopandishwa vyeo kwa wakati, saa nyingi za kazi, uhamisho wa kiholela na kusitishwa kinyume cha sheria kwa makato ya ada ya wanachama wa chama cha madaktari.

Madaktari hao wanasema wamekuwa wakipokea mishahara yao tarehe 17 au zaidi mwezi unaofuata, na mnamo Agosti 2024, malipo yao yalicheleweshwa kwa zaidi ya siku 30.

Aidha, malipo ya bima ya afya kwa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) hayajakuwa yakitumwa kwa wakati, hali inayowafanya madaktari kushindwa kutumia huduma za bima, jambo linalokiuka Sheria ya Ajira.

Madaktari wengi pia wamelalamikia kucheleweshwa kupandishwa vyeo, huku baadhi yao wakisemekana kuwa wanapitia matatizo ya kiakili kutokana na uchovu na msongo wa mawazo kazini.

Uhamisho wa madaktari umefanyika bila kuzingatia mwongozo wa usimamizi wa wafanyakazi wa serikali za kaunti wala taratibu za Tume ya Utumishi wa Umma.

Pia, marupurupu ya uhamisho hayajalipwa kwa wanaopelekwa zaidi ya kilomita 40 kutoka kituo chao cha awali.

Hata hivyo, Afisa Mkuu wa Idara ya Afya wa Kiambu, Dkt Patrick Nyaga, amekana kuwepo kwa mgogoro wa afya katika kaunti hiyo, akidai madaktari wapya wameajiriwa na baadhi ya waliogoma wamerudi kazini.

Alisema zaidi ya madaktari 90 waliokuwa kwenye mgomo wameanza kazi tena. Aidha, alisema kuwa kucheleweshwa kwa mishahara kwa baadhi ya madaktari ni kwa sababu hawajakuwa wakitoa huduma wakati wa mgomo, na kwa hivyo hawastahili kulipwa.

“Sishurutishwi na sheria kuwalipa waliogoma. Haki ya kugoma inalindwa kisheria, lakini sheria hiyo hiyo inamlinda mwajiri kutowalipa waliogoma,” alisema.

Wakati huo huo, Kaunti ya Nairobi nayo inakumbwa na changamoto baada ya wahudumu wa afya kuanza mgomo baridi, wakilalamikia kucheleweshwa kwa mishahara, kutolipwa malimbikizi ya mishahara, kutotekelezwa kwa maagizo ya Tume ya Mishahara (SRC) kuhusu nyongeza ya mshahara mwaka 2024, na kutolipwa kwa wafanyakazi wa zamani wa Huduma ya Jiji la Nairobi (NMS).

Stephen Muthama, mwenyekiti wa matawi ya Nairobi ya maafisa wa utabibu, alisema hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa idadi ya wahudumu wa afya wanaoondoka kazini, motisha duni miongoni mwa wafanyakazi waliobaki, na kusitishwa kwa huduma muhimu za afya katika vituo vya kaunti.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Madaktari (KMPDU), Dkt Davji Atellah, ametangaza kuwa kutakuwa na maandamano ya madaktari wa Kiambu mnamo Jumatatu, Oktoba 13, 2025, ili kudai uwajibikaji, heshima kwa wahudumu wa afya, na kurejeshwa kwa huduma bora na za heshima katika sekta ya afya nchini.

“KMPDU itabaki kuwa thabiti katika kutetea haki za wahudumu wa afya na kuhakikisha huduma bora kwa taifa,” alisema Dkt Atellah.