Pesa zatawala kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Kasipul
HUENDA uwezo wa kifedha ukawa kigezo cha kuamua mshindi katika uchaguzi mdogo wa Kasipul, kwani kinyang’anyiro hicho kimevutia wagombeaji matajiri.
Uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 27, 2025 unatokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Charles Ong’ondo Were aliyepigwa risasi na majambazi Aprili mwaka huu.
Japo ni wazi kwamba pesa huathiri mkondo wa siasa za Kenya, eneobunge la Kasipul ni la kipekee.
Ni eneobunge la mashambani ambako umaskini umekithiri, lakini fedha nyingi zaidi zinatumika katika kampeni.
Kwa mfano, wagombeaji wawili huru Philip Aroko na Robert Riaga, ambao ni wafanyabiashara, wameonyesha kujitolea kwao kutumia pesa nyingi kushinda kiti hicho.
Ndani ya miezi kadhaa iliyopita, wawili hao wamejijengea ufuasi kwa kufadhili mipango mbalimbali kwa pesa zao binafsi.
Kwa mfano, wamekuwa wakiwalipia karo wanafunzi kutoka familia maskini, wamekuwa wakilipa bili za hospitali na kusambaza chakula cha msaada kwa familia zisizo na uwezo kifedha.
Bw Riaga, ambaye ni mwanawe aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Waluo, Riaga Ogallo amekuwa akitumia fedha kuendesha kampeni zake kiasi cha kupewa jina la msimbo ‘Money Bior’.
Aidha, kila mara huanika mali yake mitandaoni, kwa kuweka picha za magari ghali, nyumba ya thamani kubwa yenye kidimbwi cha kuogolea na gari lenye jina lake kwenye nambari ya usajili.
Mnamo Agosti, alivutia umma baada ya kusambaza video kwenye mtandao wa kijamii wa TikTok ikimwonyesha akitua kijijini mwake kwa mkutano na madiwani wa zamani.
“Hekima zao, ushauri na kuunga mkono azma yangu kumenipa moyo na matumaini kwamba nitaibuka mshindi,” akaandika.
Kwa upande wake, Bw Aroko amejijengea himaya ya sifa kupitia wakfu wake ambao umekuwa ukiendesha mipango mbalimbali ya kusaidia jamii.
Jumatano alifika katika afisi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) eneo la Kosele akisindikizwa na msafara wa magari ya kifahari aina ya Toyota Land Cruiser Prados, kuashiria utajiri.
Hata hivyo, siku hiyo baadhi ya wawaniaji walifika katika afisi hizo kuwasilisha karatasi zao za uteuzi wakisindikizwa na misafara ya magari na pikipiki. Katika eneo kama hilo ambako umaskini umekithiri, msimu wa kampeni huonekana kama afueni kiuchumi.
Katika msimu kama huo, wapigakura wa kawaida hupokea ‘vishawishi’ vya kati ya Sh100 na Sh500 na wataalamu hupewa hadi Sh5,000.
Katika maeneo hayo ya Nyanza pesa kama hizo hujulikana kama “gonya” au “yuko jamna” na mwanasiasa asipozitoa huzomewa vikali katika mikutano yake.
Aidha, baadhi yao huzuiwa kuondoka katika maeneo ya kampeni au hata kufurushwa kwa nguvu.
Japo wagombeaji huru kama Bw Riaga na Bw Aroko wanatumia mali yao kuvutia uungwaji mkono, chama cha ODM ndicho chenye ufuasi mkubwa.
Mgombeaji wake Bw Boyd Were, mwanawe Mbunge mwendazake, anafaidi kutokana na hilo huku akifanyiwa kampeni na viongozi wakuu wa chama hicho.
Jumatano, manaibu kiongozi wa ODM Abdulswamada Nassir na Seneta Godfrey Osotsi, Katibu Mkuu Edwin Sifuna, mwenyekiti wa Kitaifa Gladys Wanga na mwenyekiti wa Baraza la Magavana Nchini Ahmed Abdullahi walijitokeza kumsindikiza Boyd alipokuwa akiwasilisha karatasi zake za uteuzi kwa maafisa wa IEBC.