Habari

Gachagua arukia Uhuru, asema hatamuomba msamaha

Na MWANGI MUIRURI October 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, amebadili msimamo wake wa awali na kusema hana sababu ya kuomba msamaha Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuhusu mgogoro wa kisiasa kati yao kabla ya uchaguzi wa 2022.

Akihojiwa na wanahabari wa redio za mashinani katika Kaunti ya Embu, Gachagua alisema kuwa tofauti zao zilikuwa za kisiasa tu na si jambo la kuomba msamaha.

“Mimi siwezi tena kuomba Uhuru msamaha. Siasa si harusi wala ibada ya Jumapili. Alikuwa anampigia debe Raila Odinga, ambaye si mzuri. Nami nilikuwa upande wa Ruto, ambaye pia si mzuri. Sasa nani alikosea mwenzake?” alisema Gachagua.

Kauli hii inajiri miezi kadhaa baada ya Gachagua kuanza kampeni ya kuomba msamaha  familia ya Kenyatta, akisema alijuta kumuunga mkono Ruto ambaye alimfanya “kuchukia mfalme wao(Uhuru).”

Baada ya kuondolewa madarakani kama Naibu Rais kupitia mchakato wa bunge mwaka 2024, Gachagua alianzisha chama kipya cha DCP na kutangaza nia ya kugombea urais mwaka 2027. Alisema hakuna kizuizi chochote cha kisheria cha azma yake kwa sababu bado ana rufaa mahakamani kuhusu kesi ya kuondolewa kwake.

Alitoa mfano wa Mbunge wa Sirisia, John Waluke, ambaye licha ya hukumu ya kifungo cha miaka 67 kwa sakata ya mahindi, aliweza kushiriki uchaguzi kwa kuwa alikuwa na rufaa mahakamani, na baadaye hukumu hiyo ikabatilishwa.

“Nami niko huru. Nina haki ya kugombea. Nitathibitisha ukweli wangu mahakamani,” alisema Gachagua.

Akiendelea kujisawiri kama kiongozi mkuu wa upinzani, alisema hana mpango wa kuunga mkono wanasiasa wa mrengo wa upinzani wasiotimiza masharti yake.

“Sitawabeba mgongoni. Wanaotaka kuwa wagombeaji wa urais lazima wakubali masharti ya muungano wa upinzani. Wasio tayari, waondoke,” alisema.

Alijisifu akisema ndiye aliyefufua upinzani alipoondolewa ofisini na kudai kuwa sauti yake ndiyo imekuwa ikizuia “kuenea kwa miradi ya Ruto” eneo la Mlima Kenya.

Kuhusu maandamano ya Gen Z yaliyotokea Juni 2024, Gachagua alimkosoa Rais Ruto kwa kutotoa ushahidi wowote licha ya kumhusisha na kupanga na kufadhili maandamano hayo.

“Niliitwa mratibu wa maandamano hayo. Mpaka leo sijaletewa ushahidi. Ikiwa serikali ina ushahidi, wauwasilishe. La sivyo, waombe msamaha,” alisema.

Gachagua pia alimkosoa Waziri wa Usalama wa Ndani wa wakati huo, Prof Kithure Kindiki, kwa kutotoa rambirambi kwa familia za vijana waliotekwa na kuuawa wakati wa maandamano.

Aliitaka serikali kukiri utekaji na mauaji ya vijana, kuomba msamaha, kuwafidia waathiriwa, na kuwafikisha wahusika mahakamani

Alishutumu serikali kwa kupuuza sera ya maendeleo ya kuanzia mashinani na badala yake kutumia “rushwa, hongo na ahadi za kijinga” kushawishi uaminifu wa kisiasa.

“Ukweli ni kuwa serikali ya sasa imewasaliti wananchi. Badala ya kuwawezesha kiuchumi, imejikita katika siasa za usaliti,” alisema.

Bw Gachagua alisema kwa sasa yeye ndiye “mlinzi mkuu wa upinzani” na akamtaka Kindiki kueleza chanzo cha mamilioni ya pesa zinazotumika kwa miradi ya uwezeshaji, akidai kuwa fedha hizo hazikuidhinishwa kwa njia halali.

Gachagua alisema kuwa kuondolewa kwake madarakani kama Naibu Rais kulipangwa na Rais Ruto pamoja na baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya kwa sababu ya msimamo wake wa kuwatetea wananchi wa eneo hilo.

Akizungumza katika mahojiano ya hivi karibuni na runinga ya KTN, Gachagua alisema ameibuka kuwa sauti ya wanyonge na sasa anachukuliwa kuwa mrithi wa Raila Odinga katika nafasi hiyo.

“Nina azma ya urais na nikichaguliwa kuwa mgombeaji urais wa upinzani ulioungana, nitashinda. Nilienda Amerika kwa mwezi mmoja na upinzani karibu ukafa,” alisema, akiwakejeli baadhi ya wenzake katika upinzani.

Aliongeza kuwa Wakenya ndio wanaomiliki na kuongoza upinzani, na kwamba yeyote atakayehujumu muungano huo atatengwa na wananchi.

Alisisitiza kuwa ndiye msemaji wa “sasa na baadaye” wa siasa za Mlima Kenya, huku akisema Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ni “alikuwa na sasa amestaafu.”