Habari

Kalonzo atawazwa kugombea urais, upinzani ukiahidi kuungana

Na NDUBI MOTURI October 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa upinzani jana walisema kuwa wako tayari kuweka kando azma  zao za kibinafsi  na kuunga mkono mmoja wao kugombea urais mwaka 2027.

Hii ni baada ya kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuteuliwa rasmi na chama chake kuwa mgombea wa urais.

Kuteuliwa kwa Bw Musyoka kumeanza mchakato wa mazungumzo mazito miongoni mwa viongozi wa upinzani kuhusu nani atakayebeba bendera ya muungano wao kumenyama na Rais William Ruto mwaka 2027.

Katika mkutano wa jana uliofanyika Uhuru Park, hotuba za viongozi zilikuwa za heshima, za kuhimiza, na za kuangalia mbele, zikionyesha kwamba wote wanaelewa umuhimu wa kile kinachowaleta pamoja.

Katika hotuba yake ya kukubali uteuzi, Kalonzo alijisawiri si tu kama mgombea wa makubaliano, bali kama chaguo linalowakilisha maadili na sera dhidi ya kile alichokitaja kama “utawala uliopoteza roho yake.” Alielezea hali mbaya nchini chini ya Rais Ruto akitaja ushuru mkubwa, deni la umma linaloongezeka, na utamaduni wa ukosefu wa uwajibikaji unaodhoofisha taasisi za nchi.

“Elimu, ambayo hapo awali ilikuwa mlango wa fursa, imekuwa mzigo. Wazazi wameingia madeni, walimu wamevunjika moyo, wanafunzi hawana uhakika wa kesho. Serikali inayotenda hivyo kwa elimu ya watoto imepoteza dira ya kimaadili,” alisema.

Alilaumu utawala wa Ruto kwa kugeuza taasisi za umma kuwa silaha za kisiasa, kuteka Bunge, kutisha vyombo vya habari, na kujaribu kuingilia uhuru wa mahakama.

Kalonzo aliahidi utawala wa “kuheshimu taifa” utakaorejesha heshima kwa shule na vyuo, kuunda ajira kupitia vituo vya teknolojia na uzalishaji viwandani, na kuanzisha tena miradi iliyokwama. Aliahidi pia kuondoa ushuru wa nyumba, kufadhili shule ipasavyo, na kurejesha utaalamu badala ya ubaguzi katika ajira.

Akizungumzia maandamano ya vijana ya mwaka jana, Kalonzo alikosoa ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji wa Gen Z na kutaja kwa huzuni kijana Bridget aliyeuawa akiwa nyumbani Kikuyu..

“Ninasema  Kenya itaibuka tena. Nawaomba vijana wapige kura kumuondoa Ruto mamlakani,” alisema, akiwataka wapiga kura kumtumia demokrasia badala ya vitendo vya ghasia.

Hotuba za viongozi wengine pia zilionyesha ari ya umoja, wengi wakiahidi kumuunga mgombeaji  atakayechaguliwa na muungano wa upinzani. Fred Matiang’i alisema, “Tutaweka kando tamaa na maslahi kunusuru nchi. Iwapo Muungano utaamua ni Kalonzo Musyoka, tutakuunga mkono. Tutabaki pamoja.”

Matiang’i alikiri mizozo ya ndani ya upinzani lakini akasema kuwa tofauti hizo ni dalili ya ubunifu wa kitaalamu, na si uhasama.

Martha Karua alimpongeza Kalonzo kwa uthabiti wake, akimtaja kama “mwanaume anayetetea wananchi wa Kenya. “Bw Ruto, hatutaruhusu ukomae kuwa dikteta,” alisema Karua, akionya kuwa Katiba inapaswa kuheshimiwa.

Eugene Wamalwa alisema umoja wa upinzani hauwezi kuvunjika: “Tunasema Ruto atakuwa rais wa muhula mmoja. Wale wanaosema tutagawanyika watasubiri muda mrefu. Tuko pamoja kumpeleka  William Samoei Ruto nyumbani.”

Rigathi Gachagua alisisimua hadhira kwa mchanganyiko wa ukali na utani. “Tutakuwa na kiongozi mmoja kukabiliana na Kasongo,.Ikiwa Kalonzo ndiye atakayechaguliwa, mimi na wafuasi wangu milioni mmoja tutamuunga mkono. Nitamfanyia kampeni.”