Ruto afichua alivyomnasa Moi wafanye handisheki
RAIS William Ruto ameonyesha weledi mpya wa kisiasa kwa kumnasa mwenyekiti wa chama cha KANU, Gideon Moi, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mpinzani wake wa kisiasa, kujiunga na serikali yake jumuishi.
Alifichua kwamba hatua hiyo pia imehusisha mazungumzo na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, jambo linaloweza kuunda upya sura ya serikali yake.
Katika hatua ambayo huenda ikazua mabadiliko ndani ya serikali, Rais Ruto jana alitangaza kuwa Bw Moi amekubali kushirikiana na serikali yake ambayo pia inajumuisha kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.
Akizungumza nyumbani kwa Bw Moi huko Kabarak, Kaunti ya Nakuru, ambako alihutubia mamia ya wafuasi wa Kanu, Rais Ruto alisema kuwa tayari amefanya mashauriano na Bw Odinga, Rais mstaafu Kenyatta na sasa Bw Moi, “ili kuwaleta pamoja viongozi kutoka mirengo yote ya kisiasa kwa lengo la kupeleka nchi mbele.”
“Huu ni mradi wa kitaifa,” alisema Dkt Ruto. “Lazima tushirikiane kama timu kuipeleka Kenya hatua inayofuata.”
Rais alieleza kuwa alichagua Kabarak, na si Ikulu ya Nakuru au Nairobi kuwa mahala pa kutangazia umma hatua hiyo kama ishara ya maridhiano ya kweli.
“Baada ya hasira za wakazi Kabarnet, nilimwambia kuwa mahala pazuri pa kutangazia umma ni hapa Kabarak,” alisema Rais, akirejelea mvutano ulioshuhudiwa Kabarnet, Baringo baada ya Bw Moi kujiondoa katika uchaguzi wa useneta unaopangwa kufanyika Novemba 27.
“Ikiwa kuna mtu wa kulaumiwa kwa mabadiliko ya moyo ya Gideon, basi ni mimi, si yeye,” alisema kwa utani. “Tunapanua serikali yetu kwa kujumuisha Kanu.”
Aliongeza: “Hili si suala la watu binafsi, si la ukabila wala maeneo. Ni kuhusu Kenya. Maendeleo nchini yamechelewa. Hatufai kuwa taifa la ulimwengu wa tatu. Nahitaji mikono zaidi, na ndio maana niliunda serikali jumuishi. Sasa nahitaji msaada wa Gideon kuipeleka nchi mbele.”
Rais Ruto alidokeza kuwa mazungumzo yao na Bw Moi pia yaligusia “mustakabali wa taifa,” ingawa hakutoa maelezo zaidi.
Kwa upande wake, Bw Moi, bila kufichua undani wa makubaliano yao, alimsifu Rais Ruto na kusisitiza kuwa umoja wa Baringo ni “muhimu kwa maendeleo ya maana.”
Alichekesha hadhira kwa kusema kuwa Ruto “alimuosha,” kabla ya kurejea kwenye msimamo wa kisiasa kwa kusema: “Tuyatimize haya kwa pamoja.”
“Handesheki” kati ya Dkt Ruto na Bw Moi inaibua kumbukumbu ya maridhiano ya 2018 kati ya Raila na Uhuru, yaliyobadili taswira ya siasa za Kenya. Hata hivyo, wakati huu, mashindano ni makubwa zaidi kwa kuzingatia kuwa uchaguzi mkuu wa 2027 uko chini ya miaka miwili tu.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Junet Mohamed, ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Odinga, aliambia Taifa Leo kuwa serikali jumuishi inaendelea kupanuka, huku akisema kuna mambo mengi yatakayowashangaza Wakenya hivi karibuni.
“Watu zaidi wanaungana nasi, na tunatarajia wengi zaidi,” alisema Bw Mohamed. “Lengo kuu ni kuunganisha taifa, kwa hivyo yeyote anayekuja, anakaribishwa.”
Alidokeza kuwa kuna mazungumzo mengi yanayoendelea kwa siri. “Kuna mikutano mingi ya usiku inayoendelea. Baadhi ya wale wanaodai kuwa wako upande wa upinzani — hivi karibuni watajikuta ndani ya Serikali Jumuishi,” aliongeza.
Mbunge wa Kimilili, Bw Dismas Barasa, ambaye ni mwanachama wa chama cha UDA cha Rais Ruto, alisema kuwa kujiunga kwa Bw Moi na kambi ya Ruto ni jambo lililochelewa mno.
“Amerejea nyumbani alipostahili kuwa tangu mwanzo. Sasa tutazingatia kumleta Matiang’i na Kalonzo,” alisema Bw Barasa.