Habari

Ogamba asema wizara inaandaa mfumo mpya wa kufadhili shule za umma

Na SAMWEL OWINO October 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAZUNGUMZO yanaendelea kati ya Wizara ya Elimu na Hazina ya Kitaifa kuhusu mfumo mpya wa kufadhili shule za umma.

Waziri wa Elimu Julius Ogamba, alifahamisha wabunge kwamba timu ya kiufundi inayojumuisha wanachama kutoka Hazina ya Kitaifa na Wizara ya Elimu kwa sasa inaandaa ratiba mpya ili kuhakikisha kuwa shule zinapokea ufadhili kwa wakati ufaao.

“Tunaoanisha kalenda ya elimu na mwaka wa kifedha wa serikali ya kitaifa ili tupate fedha wakati serikali haina shinikizo la kulipa madeni,” Bw Ogamba aliwaambia wabunge.

Alitoa maoni hayo wakati ambapo shule nyingi zimeamua kufunga mapema kutokana na uhaba wa fedha.

Akijibu maswali mbele ya kamati hiyo kuhusu kucheleweshwa kwa fedha za shule, Bw Ogamba alisema mabadiliko hayo mapya yanaweza kutekelezwa mapema mwaka ujao.

Kwa sasa, shule zinapokea ufadhili wao wa masomo kwa hivi, “Awamu ya kwanza ya asilimia 50 inatolewa katika muhula wa kwanza, awamu ya pili ya asilimia 30 katika muhula wa pili, na awamu ya mwisho ya asilimia 20 katika muhula wa tatu.”

“Hili linaweza kubadilika baada ya majadiliano ambayo yatakamilika mwishoni mwa muhula huu,” Bw Ogamba aliambia Bunge.

Katika hatua mpya, Bw Ogamba alifahamisha wabunge Alhamisi kwamba mpango huo itaruhusu Hazina ya Kitaifa kutoa fedha za ziada kwa shule wakati serikali ya kitaifa iko chini ya shinikizo la kulipa mikopo na madeni.

Waziri huyo aliwafahamisha wabunge kwamba fomula hiyo mpya itanufaisha shule pakubwa, kwani pesa hizo zitakuwa zimetengwa mara tu zikitolewa katika bajeti.

Hata hivyo, Bw Ogamba alikabiliwa na maswali magumu kutoka kwa wabunge walioeleza wasiwasi wao kwamba, ikiwa ni wiki mbili pekee hadi mwisho wa muhula wa tatu, shule nyingi bado hazijapokea ufadhili wao, jambo ambalo linaathiri utendakazi wa shule hizo.

Walidokeza kuwa shule nyingi zinapaswa kufungwa tarehe

Oktoba, 21 zikiwa zimesalia siku 10 tu, lakini bado hazijapokea fedha kutoka kwa serikali.

“Shule nyingi zinateseka. Katika eneo bunge langu, shule zinatatizika hata kununua chaki,” alisema Mbunge wa Gilgil Martha Wangari.

Waziri huyo hata hivyo alihusisha kucheleweshwa kwa fedha na uhakiki unaoendelea wa shule ambao alisema utakamilika wiki ijayo Jumatano.