Makala

Ruto atupa mahasla kuendea ‘madynasty’

Na BENSON MATHEKA October 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto alipokutana na mwenyekiti wa KANU, Gideon Moi na kutangaza hadharani handisheki yao huko Kabarak, halikuwa tu tangazo la kawaida la kisiasa.

Yalikuwa mabadiliko ya msimamo wa kisiasa wa kiongozi ambaye aliwahi kujitangaza, mara si moja, kuwa mpinga mazoea ya madaraka ya kifamilia almaarufu ‘dynasty’.

Kabla ya uchaguzi mkuu mwaka wa 2022, Rais Ruto aliendesha kampeni iliyosheheni kauli mbiu ya “Hustler dhidi ya Dynasty” – alijisawiri kama mtetezi wa Wakenya wa kawaida dhidi ya familia za kisiasa zilizotawala kwa miongo kadhaa.

Alijenga umaarufu wake kwa msingi wa kupinga kile alichokiita ‘ukiritimba wa kisiasa’ wa familia za Kenyatta, Odinga na Moi.Jumamosi, Ruto mwenyewe alifichua kwamba amezungumza na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta na akatangaza kuwa Bw Moi amekubali kushirikiana na serikali yake ambayo pia inajumuisha kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Akizungumza nyumbani kwa Bw Moi huko Kabarak, Kaunti ya Nakuru, ambako alihutubia mamia ya wafuasi wa Kanu, Rais Ruto alisema kuwa tayari amefanya mashauriano na Bw Odinga, Rais mstaafu Kenyatta na sasa Bw Moi, “ili kuwaleta pamoja viongozi kutoka mirengo yote ya kisiasa kwa lengo la kupeleka nchi mbele.Lakini handisheki zake na wanasiasa hawa zimeibua gumzo.

Kwa wengi, ni hatua inayokinzana moja kwa moja na ujumbe wake wa kampeni ya 2022.Katika kipindi cha kampeni za uchaguzi wa 2022, Ruto aliwashambulia vikali viongozi wa vyama vya kisiasa wanaotoka kwenye familia tajiri za kisiasa, akisisitiza kwamba Kenya inahitaji mageuzi na uongozi mpya unaotokana na tabaka la chini la kiuchumi.

Alijipamba kama “mtu wa chini” aliyeinuka kwa bidii hadi juu, tofauti na “wana wa kifalme wa kisiasa” waliopokezana madaraka kwa vizazi. “Hivi ni vita kati ya wana wa maskini dhidi ya wana wa wafalme,” alikuwa akisisitiza wakati huo.Lakini sasa, kwa kukumbatia ushirikiano wa kisiasa na Moi baada ya Odinga na kuashiria anaendelea kuzungumza na Uhuru, Ruto ameonekana kuvuka mstari aliouweka mwenyewe.

Moi alitangaza wazi kuwa yuko tayari kushirikiana na serikali ya Ruto, na tayari amejiondoa katika uchaguzi mdogo wa Baringo na Ruto amekiri kwamba Moi atajiunga na Serikali Jumuishi.

Kwa wachambuzi wa siasa, handisheki hii haiwezi kutazamwa kwa jicho la kawaida. Kuna wanaoiona kama mkakati wa kisiasa unaolenga kuunganisha nguvu kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Kwa kuingiza vyama vya upinzani serikalini kupitia Serikali Jumuishi, Ruto anaonekana kuunda kuta imara za kisiasa kuzuia mpinzani yeyote kumshinda kwa urahisi. “Ruto anatekeleza siasa ya kujilinda kisiasa.

Kukumbatia Gideon Moi si jambo la ghafla, ni mpango wa muda mrefu wa kupunguza upinzani mkali kutoka kwa vigogo wa zamani na hasa familia za kifalme alizolaani wakati wa kampeni iliyopita,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Lakini kwa baadhi ya wafuasi waliomchagua Ruto kwa msingi wa kupiga vita familia hizo, mabadiliko haya ni kama usaliti wa kisiasa.

Wengi wao wanahisi kama kauli mbiu ya “Hasla” ilikuwa ni mbinu ya kisiasa ya kujipatia kura tu na wala haukuwa msimamo wa kweli. “Wengi walimpigia kura Ruto kwa sababu alionekana tofauti na hizo familia za kifalme. Sasa anashirikiana nazo. Hii si haki kwa waliomwamini,” aongeza Dkt Gichuki.

Katika mazingira ya sasa, asema mchambuzi huyo, Rais Ruto anavutana na pande mbili tofauti: upande wa kutekeleza sera zinazolenga kuwainua wanyonge, na upande mwingine wa kushirikiana na wale aliowashutumu kuwa ndio chanzo cha ukosefu wa usawa wanaolenga kutimiza maslahi yao.

Kwa ufupi, asema Gichuki, Ruto amejiunga na dynasty na analenga kulinda maslahi yake. Hili linaweka serikali yake katika hali ya mkanganyiko wa maadili ya kisiasa.Mchanganuzi wa siasa Peter Kasoa naye anasema Rais anaenda kinyume na kile alichohubiri wakati wa kampeni kwa sababu ya kuweka kinga ya kisiasa kwa kuwa mengi yamebadilika tangu alipoingia mamlakani.

“Wakati mmoja alionekana kubomoa mfumo wa urithi wa kisiasa, lakini sasa anaonekana kuwa sehemu ya mfumo huo. Matendo yake yanaanza kufifisha tofauti iliyokuwa kati yake na viongozi wa zamani. Haya yote ni katika juhudi za kutafuta kinga ya kisiasa kwa kuwa mengi yamebadilika tangu alipoingia mamlakani,” asema.

Katika siasa, asema, viongozi hubadili misimamo ili kudumu madarakani au kupata ushawishi zaidi.