Habari

Wazazi walia kuadhibiwa visivyo kupitia faini za juu baada ya migomo ya wanafunzi

Na MERCY SIMIYU October 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAZAZI wa shule mbalimbali wamelalamika kuwa wanatozwa faini ya juu kila mara ambapo kuna mgomo na mali ya shule huchomwa au kuharibiwa.

Hivi majuzi wazazi wa Shule ya Wavula ya Litein walikipata baada ya kila mzazi kuamrishwa alipe Sh49,000 kugharimia uharibifu ambao ulitokea shuleni humo baada ya mgomo wa wanafunzi.

Kesi kuhusu suala hilo ipo mahakamani na wanafunzi nao wanaendelea kuwa nyumbani huku masharti makali ya kumaliza deni lote la karo pia yakiwekwa na uongozi wa shule hiyo.

Katika Shule ya Wavulana ya Gatunguru, wazazi walitakiwa walipe Sh25,000 kila mmoja kama faini kutokana na uharibifu uliosababishwa na mgomo uliotokea Septemba 7, 2025.

Bodi simamizi ya shule hiyo pia iliwaamrisha wazazi wamalize deni lote la karo kabla ya watoto wao kuruhusiwa kurejea darasani.

Katika Shule ya wavula ya Tengecha, Kaunti ya Kericho, wazazi waliambiwa walipe faini ya Sh5,500 baada ya wanafunzi kugoma na kuharibu mali ya shule.

Hali ilikuwa hiyo hiyo AIC Chebisaas ambapo kila mwanafunzi alilipa Sh5,000 kufidia hasara iliyotokana na mgomo wa Julai 19, 2025.

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Nchini (KNUT) Collins Oyuu alisema kuwa ingawa ni lazima wanafunzi wagharimie uharibifu wa mali ya shule kunapotokea mgomo, wazazi hawastahili kutozwa kiwango cha juu cha fedha.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Muungano wa Kitaifa wa Wazazi (NPA), baadhi ya shule huweka tu faini bila kushauriana na wazazi na hilo huwatundika wazazi mzigo mkubwa ilhali uchumi ni mgumu.