Makala

Kura ya Magarini kuleta kumbukumbu ya Msambweni iliyoumiza vibaya Uhuru na Raila

Na WAANDISHI WETU October 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HISTORIA inajirudia katika uchaguzi mdogo wa ubunge Magarini, ambapo aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua anatarajiwa kupimana nguvu na Rais William Ruto.

Miaka mitano iliyopita, hali kama hii ilishuhudiwa katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Msambweni, wakati Dkt Ruto, akiwa naibu rais, alikabiliana dhidi ya mgombeaji wa ODM aliyeungwa mkono na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.

Dkt Ruto wakati huo alimkaidi Rais Kenyatta, kwa kumuunga mkono mgombea huru Feisal Bader dhidi ya mgombea wa ODM, Omar Boga.

Chama cha Jubilee, kilichoongozwa na Rais Kenyatta wakati huo, kilikuwa kimeamua kutoweka mgombeaji, badala yake kikiunga mkono ODM ya Raila Odinga kwa msingi wa makubaliano ya “Handshake”.

Bw Bader aliibuka mshindi, na kutoa taswira kuhusu uwezekano wa vuguvugu la ‘Hustler’ kudidimiza ushawishi wa nguvu za utawala.

Mwaka huu, katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Magarini, Kaunti ya Kilifi, chama cha Rais Ruto cha UDA kilijiondoa katika kinyang’anyiro hicho kikimuunga mkono aliyekuwa Mbunge wa ODM, Harrison Kombe, chini ya makubaliano ya ‘Broad-based’ na Bw Odinga.

Uamuzi huu ulimfanya Bw Stanley Kenga, aliyekuwa mgombeaji wa UDA katika Uchaguzi Mkuu wa 2022 na aliyefanikiwa kupinga ushindi wa Bw Kombe mahakamani, kuhamia chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Bw Gachagua.

Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, alisema kuwa katika kikao kati yake, Rais, na Bw Odinga, waliamua kwamba aliyekuwa mbunge, Bw Kombe, ndiye angepeperusha bendera ya ‘Broad-based’. Hata hivyo, uamuzi huo haukupokelewa vyema na Bw Kenga, licha ya madai kwamba alipewa nafasi ya kazi serikalini na akakataa.

“Kiti hiki kilikuwa kinashikiliwa na Bw Kombe; ni haki kumpa nafasi akamilishe muhula wake. Najua Bw Kenga alishangaa kwa nini hakuchaguliwa, lakini ukweli ni kwamba Bw Kombe alikuwa ameanza kazi na amefika katikati,” alisema Bw Mung’aro.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Owen Baya, alisema Chama cha United Democratic Alliance (UDA), Pamoja African Alliance (PAA), na vyama vyote vinavyohusiana na Kenya Kwanza vitamfanyia kampeni Bw Kombe.

PAA haikuweka mgombeaji baada ya Bw Michael Kingi, aliyewania kwa tiketi ya chama hicho mwaka 2022, kuteuliwa kuwa mmoja wa wajumbe wa Tume ya Mishahara na Marupurupu mwezi Agosti.

Kauli kama hizo pia zilitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara nchini, Bi Aisha Jumwa, ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais Ruto katika Kaunti ya Kilifi.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwania, Bw Kenga alikashifu makubaliano ya kisiasa yanayoshawishiwa na viongozi serikalini.

Alieleza matumaini kwamba IEBC na taasisi husika zingehakikisha uwazi na kulinda haki za wananchi wa Magarini.

“Hatuko kwenye siasa kufanya biashara. Ninaamini kila mtu ana haki ya kushiriki uchaguzi kama mpiga kura au mgombeaji. Nimeamua kushiriki katika uchaguzi mdogo wa Magarini,” alisema Bw Kenga.

IEBC imeidhinisha wagombeaji 10 kushiriki uchaguzi huo mdogo katika eneo la Magarini. Jumatano, tume iliidhinisha wagombea saba na watatu waliobaki wakaidhinishwa Alhamisi.

Ripoti za Valentine Obara, Winnie Atieno na Maureen Ongala