Waliopoteza watoto ajali ya boti Tudor Creek waishiwa subira shughuli ya uokoaji ikijikokota
SHUGHULI ya kusaka vijana watatu ambao hawajapatikana baada ya boti kuzama katika Bahari Hindi wakati wa mashindano ya uendeshaji boti yaliyoandaliwa na shirika la East African Ocean jijini Mombasa Jumapili iliingia siku yake ya tatu hasira zikipanda huku familia zikitaka waandalizi kuwajibikia kisa hicho.
Mkasa huo ulitokea Ijumaa katika Tudor Creek wakati wa awamu ya mwisho mashindani hayo. Washiriki 19 kati ya 22 kutoka kwa kundi la vijana la Kijiweni Youth Uplift waliokolewa baada ya boti moja kuzama ikiwa mbioni.
Hata hivyo, wanaume watatu – Steven Karembo Ngowa, 23, Tom Wanyonyi, 21, na Caleb Otieno, 21, bado hawajapatikana.
Familia za vijana hao zimekuwa zikipiga kambi ufuoni Tudor Creek tangu Ijumaa wakiwatazama wapiga mbizi kutoka Jeshi la Wanamaji, Huduma za Ulinzi Maji Nchini (KCGS) na wahisani wakiendesha msako katika eneo la mkasa.
“Kakangu anaitwa Steven, kwa jina maarufu Lavosty. Ndiye mvulana wa pekee katika familia yetu. Mkewe ni mjamzito. Amekuwa akifanya kazi za sulubu kulisha familia yake,” akasema Bi Lilian Karembo, machozi yakimtoka.
Mamake, Steven, Bi Joyce Damah alilia wakati wote alipokuwa akizungumza na Taifa Leo.
“Hii ni siku ya tatu na sijaona mtoto wangu na hakujua kuogelea, ninahisi uchungu. Tunataka kukutana na waandalizi wa shughuli hii kwa sababu hawajawasiliana nasi tangu mkasa huo ulipotokea,” akasema.
Juhudi za uokoaji zilipokuwa zikiendelea jana, familia kadhaa zilikuwa zikihoji hatua za kiusalama ziliwekwa na waandalizi, zikidai washiriki hawakuwa na jaketi za usalama.

Bi Jemimah Akinyi, aliyempoteza mpwa wake Caleb Otieno, aliuliza ni kwa nini walivalia jaketi za usalama wakati wa mazoezi lakini hawakuzivaa siku ya mashindano.
“Tunataka waandalizi kutupa maelezo kuhusu suala hili,” akasema.
Bi Akinyi akaongeza, “Tumekuwa hapa tangu Ijumaa, na hatujapata habari zozote. Mbona maafisa zaidi wa usalama ndio wanaletwa wala sio wapiga mbizi? Hatutaki kushiriki fujo, tunataka haki kwa watoto wetu.”
Alisema Caleb alikuwa vijana mwenye bidii aliyeishi katika mtaa wa mabanda wa Bangladesh aliyejichumia mapato kwa kufanya kazi katika maeneo ya mijengo.
“Akipata pesa alikuwa akininunulia mkate na maziwa akiniambia Mama, nimeanza kujipata pesa, mamake Janet Adhiambo akaeleza.
“Mbona waliwaruhusu watoto wetu kuingia majini bila mavazi ya kujikinga, eti kushindania Sh300,000 pekee?”
Kwa upande wake Bi Lydia Nyange, anahisi uchungu kwa kumpoteza kitinda mimba wake, Tom Wanyonyi, almaarufu Tommy Lee Sparta.
“Mtoto wangu hakujua kuogelea,” akasema.
“Alikuwa mwanakandanda chipukizi na alianza kusakata soka akiwa na umri wa miaka miwili. Nani aliwasafirishwa kutoka Bangladesha hadi Tudor Creek?” akauliza huku akilemewa na machungu.