Maasi yamuandama Gachagua Mlimani kina mama wakiandamana Kirinyaga
MAASI yameanza kumwandama aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua Mlima Kenya baada ya mamia ya akinamama kuandamana Jumatatu, Oktoba 13, 2025 Kaunti ya Kirinyaga, wakimshutumu kwa kumkosea heshima Gavana Anne Waiguru.
Wakiwa wamebeba mabango, akinamama hao walijibwaga kwenye barabara ya Kutus ambapo walitoa wito kwa wenzao kutoka pembe zote za nchi wakatae siasa za Bw Gachagua na chama chake cha DCP.
Maandamano hayo yalizingirwa na taharuki kuu huku yakisababisha uchukuzi kusitishwa kwenye barabara ya Embu-Kutus.
Baadhi wakiwa wamejilaza barabarani na wengine wakiwasha moto uliosababisha moshi kubwa kufuka, akinamama hao pia waliapa kuwa watamfunza Bw Gachagua adabu ambayo hatasahau kwenye maisha yake ya kisiasa.
Walisema Bw Gachagua alionyesha kuwa hawaheshimu wanawake kwa kumpiga vita Bi Waiguru.
“Kama wanawake wa Kirinyaga, tumemkasirikia sana Gachagua, amwache Waiguru afanye kazi yake na amheshimu,” akasema Bi Wanjiru Wanjohi.
Wengi wao walisema wao ndio walimchagua Bi Waiguru na ndio wanastahili kuamua mkondo wa siasa anaouchukua badala ya Bw Gachagua.
“Tunamwambia Gachagua ajaribu kumdhalilisha Waiguru tena. Gachagua amkome Waiguru na akae kwake Wamunyoro kwa sababu Kirinyaga ina wenyewe,” akasema mwaandamanaji mwingine.
Wanawake hao walisema hawamtambui Bw Gachagua kama kigogo wa siasa za Mlima Kenya na wakamwambia asahau kura zao.
“Hatutamruhusu mtu yeyote aanzishe vita dhidi ya Gavana. Bw Gachagua asahau kura zetu wala si kiongozi wetu,”akasema mwingine.
Akiwa katika ziara Kaunti ya Embu akiwa ameandamana na viongozi wengine wa upinzani, Bw Gachagua alimtaja Bi Waiguru na Gavana Cecily Mbarire kama viongozi wasaliti ambao wanaotumiwa kuwagawanya wakazi wa Mlima Kenya.
Aidha, alitoa wito kwa wakazi wa Embu wasiwachague viongozi ambao wanaunga mkono utawala wa sasa.