MAONI: Tanzania yaelekea kichakani, Samia akumbatie demokrasia kuongoza
HIVI Tanzania inaelekea wapi? Kwani serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan haijui ukandamizaji huwageuza raia sugu kiasi cha kutoogopa mauti?
Huku zikisalia wiki mbili unusu hivi kabla ya taifa hilo kufanya uchaguzi mkuu, wasiwasi unaendelea kutanda kote kote kutokana na visa vya utekaji na mateso wanayofanyiwa wakosoaji wa serikali.
Wengi wametekwa, wakauawa, baadhi wakatoweshwa wasijulikane waliko, lakini mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Mama Samia bado yanapamba moto.
Na, kwa kuwa ujasiri si ukosefu wa wasiwasi, Watanzania wasiotarajiwa kufunguka kikamilifu kuhusu masuala ya demokrasia wamekataa kunyamazishwa, wakatokea kimasomaso kuikemea serikali yao, wakarekodi video na kuzipakia mtandaoni.
Mwathiriwa wa dhuluma wa hivi karibuni zaidi ni Bw Humphrey Polepole, ambaye alikuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba hadi alipojiuzulu miezi michache iliyopita ili kuonyesha kutoridhika na jinsi Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilivyomteua mgombea wake wa urais – Bi Samia.
Kwa mujibu wa taarifa, Bw Polepole alitekwa nyara Jumatatu katika tukio lililoashiria kuwa la matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa kuwa damu ya mateka huyo ilichuruzika kutoka chumbani alimopatikana hadi lango la nyumba yake.
Bw Polepole – ambaye kwa kuweza kujificha kwa muda mrefu huku akitema cheche kali dhidi ya utawala wa sasa, wengi waliamini alikuwa nje ya nchi – amekuwa mwiba kwa chama chake cha CCM wakati ambapo kinafanya kila juhudi kunata madarakani.
Inaaminika ujasiri wake na msisitizo kwamba, ni sharti chama hicho kijirudi kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika umewachochea wengi wakaishia kupoteza imani nacho kabisa.
Watanzania, na yeyote anayefuatilia matukio nchini humo, walishtuka pale, siku chache kabla ya balozi huyo kutekwa, ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliyejitambulisha kama Kapteni Tesha alihimiza wakuu wake watwae mamlaka na kuidhibiti nchi.
Ni rahisi kumpuuzilia mbali mwanajeshi huyo aliye mafichoni kama yatima wa kisiasa wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, John Pombe Magufuli, hasa kwa sababu alisisitiza kuwa kifo cha marehemu Magufuli kinapaswa kuchunguzwa.
Ni rahisi pia kumpuuzilia mbali Balozi Polepole kwa sababu alikuwa msiri wa marehemu Magufuli, na yeye pia aliwahi kusema kuwa rafiki yake huyo hakufa kifo cha kawaida.
Lakini tutamchukuliaje aliyekuwa mpinzani mkuu wa Magufuli, Tundu Lissu, kigogo wa upinzani aliyebambikiziwa makosa ya uhaini kwa kudiriki kusema hakutakuwa na uchaguzi iwapo kwanza Katiba ya nchi haitabadilishwa?
Tanzania pana tatizo; watu wote hao hawawezi kuwa wabaya, eti Mama Samia ndiye aliyetukuka.