Habari

Dereva wa ‘takataka’ apigwa faini ya Sh100,000

Na RICHARD MUNGUTI October 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

DEREVA wa Mbunge wa Kibra Peter Orero ambaye alinaswa kwenye kamera akiendesha gari upande usiofaa wa barabara, Jumatatu alitozwa faini ya Sh100,000 au miezi 12 gerezani.

Mwanahabari wa CNN Larry Madowo alimnasa dereva huyo George Oduor pamoja na mbunge huyo wakiendesha gari upande usiofaa wa barabara ya Oloitoktok mnamo Oktoba 9 saa nane na dakika 40 mchana. Alikuwa akijaribu kukwepa msongamano uliokwepo kwenye barabara hiyo.

Oduor alimwambia Bw Madowo aende amripoti kwa Rais William Ruto kisha akamdhalilisha zaidi kwa kumwita ‘takataka’.

Oduor alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi Rose Ndombi kwa kosa la kuhatarisha maisha ya watumiaji wengine wa barabara.

Mahakama iliambiwa kuwa sheria inahitaji wanaotumia barabara watumie lugha ya adabu tena yenye heshima. Hakimu aliombwa amwaangushie dereva huyo adhabu kali ili iwe funzo kwake na kwa wengine wenye nia ya kuvunja sheria za trafiki.

Oduor naye aliomba hakimu amwonee imani kwa sababu alikuwa akimwendesha mbunge wakati wa tukio hilo. Pia alisema kukiri makosa yake kulikuwa kwa nia njema na hangerudia kufanya hivyo.

Hakimu alitambua kuwa alihatarisha maisha ya watu wengi wanaotumia barabara na akamwangushia faini ya Sh100,000.

“Mshtakiwa amesikitikia makosa yake na naomba alipe Sh100,000 au atumikie kifungo cha miaka 12 gerezani,” akasema Bi Ndombi.

Mahakama pia ilimpa siku 14 akate rufaa kuhusu hukumu hiyo.