Afueni wanawake Lamu wakisajiliwa makurutu wa KDF mara ya kwanza tangu 2019
ILIKUWA ni afueni kwa mabinti wa kisiwa cha Lamu Jumatatu baada ya shughuli ya kusajili makurutu kuingia jeshini (KDF) kujumuisha jinsia ya kike.
Kwa zaidi ya miaka sita iliyopita, mamia ya wanawake waliokuwa wakijitokeza kwenye bustani ya Kibaki mjini Lamu kutafuta nafasi kujiunga na KDF walikuwa wakivunjika moyo kwani hawakuruhusiwa kushiriki zoezi hilo.
Hii ilitokana na sababu kuwa hakukuwa na nafasi zilizotengewa jinsia ya kike miaka hiyo.
Jumatatu hali ilikuwa tofauti kwani makurutu wa kike waliojitokeza waliruhusiwa kushiriki mazoezi na kutafuta nafasi ya kusajiliwa kuhudumia jeshi la Kenya.
Baadhi ya waliozungumza na Taifa Leo hawakuficha furaha yao wakisema kuruhusiwa kwa jinsia ya kike ni mwamko mpya Lamu.
Bi Khadija Omar, 23, alisema japo alishindwa mapema na hata kutolewa kwenye mbio za kutafuta nafasi ya kusajiliwa katika KDF, furaha yake ni kwamba wanawake waliruhusiwa kushiriki.
“Niko mchanga bado nikiwa miaka 23 pekee. Nitajikaza kufanya mazoezi ili mwaka ujao nifaulu mbioni na kujiunga na KDF. Hiyo ndiyo azma na fahari yangu,” akasema Bi Omar.
Mohamed Ali, mmoja wa makurutu waliojitokeza kisiwani Lamu lakini akatolewa mapaema kwa kukosa kuafikia gredi inayokubalika ya D katika KCSE, aliwasifu maafisa wa usajili kwa uwazi na uwajibikaji.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo Jumatatu, Afisa Mkuu wa Usajili wa Makurutu wa KDF Lamu Luteni Kanali Eliud Nangole alithibitisha kuzingatia jinsia zote katika usajili huo.
“Makurutu karibu 110, wakiwemo wanawake kwa wanaume wamejitokeza leo. Tunazingatia kuteua jinsia zote bila ubaguzi, ukabila, dini au rangi. Usajili unaendelea vyema na tunatarajia kuukamilisha jioni,” akasema Bw Nangole.
Jumanne, shughuli ya kusajili makurutu itafanyika mjini Mpeketoni ilhali Jumatano ikikamilika kisiwani Faza, Lamu Mashariki.