Uharibifu uliotokea Shule ya Wavulana ya Litein wanafunzi walipofanya mgomo mwezi jana. Picha|Winny Chepkemoi
HATIMA ya wanafunzi 400 wa Kidato cha Nne wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Litein katika Kaunti ya Kericho bado haijulikani baada ya Mahakama Kuu kukataa kuamuru mkuu wa shule hiyo kuwarudisha shuleni.
Wanafunzi hao wanatarajiwa kufanya mtihani wa kitaifa wa KCSE wiki ijayo.
Hata hivyo, shule hiyo yenye wanafunzi 2,000 ilifungwa kufuatia ghasia zilizotokea Septemba 21. Wazazi wanatakiwa kulipa Sh69.5 milioni ili kufadhili ukarabati wa shule hiyo.
Badala ya kufuta uamuzi wa kufunga shule hiyo, Jaji Joseph Sergon alitambua kesi hiyo iliyowasilishwa na shirika la haki za binadamu Sheria Mtaani na Shadrack Wambui kuwa ya dharura.
Aliagiza kesi hiyo kutajwa Oktoba 23 ili kupangiwa tarehe ya kusikilizwa. Hii itakuwa ni siku mbili baada ya kuanza kwa mtihani wa KCSE.
Shirika hilo la haki limepinga agizo la usimamizi wa shule kwa kila mzazi kulipa Sh69,929,610.
Kesi hiyo ilipowasilishwa mbele ya Jaji Sergon mnamo Oktoba 13, aliwaelekeza mawakili Danstan Omari na Shadrack Wambui kuwapatia washtakiwa stakabadhi za kesi hiyo ndani ya siku tatu.
Washtakiwa ni Bodi ya Usimamizi ya Shule ya Upili ya Wavulana ya Litein, Mkuu Mkuu wa shule, pamoja na Baraza la Mitihani la Kitaifa Kenya (KNEC), Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba, Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti ya Kericho, na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC).
Jaji pia aliamuru pande zote kuwasilisha hoja zao za maandishi ndani ya siku saba.
“Walalamishi wamewasilisha kesi hii kwa mujibu wa Kifungu cha 22(2) na 258(1) cha Katiba kulinda haki za kibinafsi za wanafunzi kupata elimu,” alisema Bw Omari katika stakabadhi za mahakama.
Sheria Mtaani limetaja kiwango cha fidia cha Sh69.5 milioni kinachodaiwa na shule hiyo kuwa kisicho cha haki na kisichotegemea makadirio ya gharama yaliyo hakikiwa.
Mawakili waliambia mahakama kuwa mgomo wa mwezi uliopita ni wa tatu katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, jambo linaloashiria matatizo ya mara kwa mara ya ustawi na usimamizi yasiyotatuliwa katika mazingira ya shule.
“Wanafunzi wameonyesha hofu ya kweli ya kubaguliwa, kulipiziwa kisasi, au kuhukumiwa vibaya iwapo watapinga maamuzi ya kiutawala mmoja mmoja,” akasema Bw Omari.
Kuhusu ada kubwa za ukarabati, wazazi wamedai kuwa maombi yao ya ripoti huru ya tathmini, maelezo ya kina ya uharibifu, au ukaguzi wa gharama hayakuzingatiwa.
Wanaomba mahakama kuzuia shule na maajenti wake kutekeleza au kukusanya ada hizo.
Wazazi pia wanaomba mahakama kuamuru shule kutozuia au kuchelewesha kurudishwa kwa mwanafunzi yeyote kati ya 2,000 kutokana na kutolipa ada hiyo.
Zaidi, wazazi wanaomba mahakama kuzuia juhudi za kufuta usajili wa shule ya hiyo kama kituo cha mtihani cha KNEC kutokana na hali zilizojitokeza.