Habari

Ruto arudi darasani kusomea masuala ya AI

Na MERCY SIMIYU October 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto amejisajili kusomea shahada ya uzamili katika taaluma ya Akili Unde (AI) katika Chuo Kikuu cha Open University nchini (OUK).

Rais Ruto alisema hatua hiyo inalenga kuongeza uelewa wake kuhusu masuala ya teknolojia na athari zake kwa utawala, biashara na jamii.

Akizungumza akiwa Konza Technopolis wakati wa uzinduzi wa awamu ya kwanza ya miundombinu, Rais Ruto alisema uamuzi huo ni hatua ya kibinafsi ya kuelewa teknolojia ambayo inabadilika kwa kasi.

“Nimejisajili kama mwanafunzi wa AI kwa sababu ninataka kuielewa. AI inasumbua. Itabadilisha jinsi tunavyofanya biashara, jinsi tunavyoendesha serikali, na jinsi tunavyotoa huduma kama vile afya na elimu,” alisema.

Masomo hayo  ni ya miaka miwili  na yanatolewa kikamilifu mtandaoni.

Kwa kuwa na shughuli nyingi, Rais sasa atalazimika kupanga muda wa kuhudhuria masomo, kufanya kazi pamoja na kufanya mitihani.

Mpango huo unagharimu Sh187,500 kwa mwaka wa kwanza na Sh86,000 kwa mwaka wa pili.

Rais alibainisha kuwa ulimwengu unaingia katika enzi mpya ya kiteknolojia ambayo inawahitaji viongozi kuwa na uelewa kuhusu masuala ya uvumbuzi na kuwa na uzoefu hitajika.

Alisema uamuzi wake wa kurejea darasani ni ishara ya mabadiliko ya mawazo yanayohitajika ili kuendana na maendeleo ya kiteknolojia duniani.

Alisema viongozi wanafaa kutenga muda ili kufahamau masuala ya teknolojia.

“Akili Unde itaongoza dunia katika siku zijazo. Sisi katika uongozi lazima tuendelee kujifunza ili tuweze kufanya maamuzi sahihi katika ulimwengu unaobadilika haraka,” alisema.

Alifichua kuwa serikali imejitolea kupanua upatikanaji wa elimu kwa bei nafuu kupitia majukwaa yanayoendeshwa na teknolojia kama vile OUK.

“Kufikia 2026, Chuo Kikuu cha Open University kitasjili wanafunzi 100,000,” alisema Rais.

“Kitakuwa chuo kikuu kikubwa zaidi nchini Kenya. Tumewekeza rasilimali ili kufanya masomo kuwa ya bei nafuu. Gharama ya kozi za mtandaoni itakuwa chini ya kile ambacho vyuo vikuu vingine vinatoza,” alisema.

Pia alipongeza maendeleo ya OUK, ambayo alisema ina jukumu muhimu katika kupanua upatikanaji wa elimu kupitia teknolojia.