Ni sisi tuko! Cape Verde wafuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kabisa
KOCHA Pedro Brito wa timu ya taifa ya Cape Verde amesema kikosi chake kiko tayari kupambana na miamba nchini Amerika mwaka ujao, baada yao kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kabisa.
Wanavisiwa wa Cape Verde waliweka historia ya kuwa nchi ndogo ya kwanza kufuzu kwa Kombe la Dunia, ushindi ambao umeifanya kuwa nchi ya pili katika historia kufuzu kwa mashindano hayo makubwa zaidi duniani.
Kufikia Jumanne, mataifa ya bara Afrika ambayo yalikuwa tayari yamefuzu ni Algeria, Cape Verde, Egypt, Ghana, Morocco na Tunisia.
Nafasi zingine nne zilikuwa ziamuliwe katika mechi za Jumanne usiku, kufikisha jumla ya mataifa tisa ya Afrika yatakayonogesha kindumbwendumbwe hicho cha mwaka ujao.
Kombe la Dunia 2026 litashirikisha timu 48 na litaandaliwa kwa pamoja na mataifa ya Amerika, Canada na Mexico.
Awamu ya kwanza ya mchujo wa mataifa ya bara Afrika imekamilika huku washindi wa makundi tisa wakijikatia tikiti ya moja kwa moja.
Timu zitakazomaliza nambari mbili katika kila kundi zitapigwa tathmini ili kubaini nne bora miongoni mwao.
Ni hizo zitakazoingia katika droo ya awamu ya pili ya mchujo, ambapo mshindi atawakilisha Afrika katika mchujo baina ya mabara mwaka ujao.
Kikosi hicho cha kocha Pedro Brito kilifuzu baada ya kutandika Eswatini 3-0 kwenye mechi ya mwisho ya Kundi D iliyosakatiwa Jumatau.
Baada ya kutofungana katika kipindi cha kwanza, Cape Verde maarufu kama Blue Sharks walirudi uwanjani wakiwa na ari na kupata mabao hayo kupitia kwa nahodha Dailon Livramento kabla ya Willy Semedo na Tavares Stopira kuongeza mawili.
Kutoka Praia hadi visiwa vya Sao Vicente na Sal, wananchi wa taifa hili la Afrika Magharibi walijitokeza kwa wingi barabarani kufurahia ushindi huo baada ya mwamuzi kupuliza firimbi ya kumaliza mchezo.
“Tumeota ndoto hii kwa miaka mingi. Ushindi huu ni kwa ajili ya kila mwananchi wa taifa hili aliye hapa nchini na nje. Hii ni ndoto iliyotimia. Soka imetuleta pamoja kama taifa,” alisema Livramento baada ya mechi hiyo iliyochezewa Esadio Nacional de Cabo Verde.
Baada ya kumaliza mechi zake 10 za kundi, Cape Verde wamemaliza kileleni na pointi 23, baada ya kushinda mara saba, kutoka sare mara mbili na kushindwa mara moja pekee, matokeo ambayo yameshangaza mashabiki wengi duniani.
Baada ya kutoka sare 3-3 na Libya, ilikuwa lazima washinde Eswatini ili kufuzu moja kwa moja.
Brito ambaye amekuwa na timu hiyo tangu 2021 alisema ndoto yao ilitimia kutokana na nidhamu na umoja wa wachezaji.
“Sisi ni taifa dogo lakini umoja wetu ni mkubwa. Timu ilijiamini na tumefaulu baada ya safari ndefu. Kufuzu ni mwanzo tu. Tunataka kwenda huko kupambana, wala si kushiriki tu,” alisema Brito baada ya mechi hiyo iliyohudhuriwa na zaidi ya mashabiki 15,000.
Kwa ufanisi huo, Cape Verde ambayo ni nchi ya watu wapatao 600,000 imejiunga na Iceland ambayo ndiyo nchi ndogo pekee iliyoandika historia kama hiyo.
Mara tu baada ya mechi kuamlizika, magari yalipiga honi, huku miziki ikisikika kwa sauti ya juu kote mitaani.
Rais Jose Maria Neves aliungana na wananchi kufurahia ushindi huo wa kihistoria huku akitumia wakati huo kutuma ujumbe wa pongezi kwa wachezaji, akiutaja ushindi huo kuwa wa imani, uvumilivu na umoja wa taifa zima.
Akizungumza kuhusu kufuzu huko kwa kihistoria, Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) Patrice Motsepe alisema litakuwa somo kwa mataifa mengine madogo kwamba bidii na umoja vinaweza kuzaa matunda.
Kocha Brito alisema timu yake itaanza kushiriki mechi za kirafiki mwishoni mwa mwaka huu kwa lengo la kuimarika kabla ya fainali hizo za Kombe la Dunia.
Matokeo ya mechi zilizochezwa Jumatatu
Equatorial Guinea 1-1 Liberia, Sao Tome and Principe 1-0 Malawi, Mauritius 0-0 Libya, Loseotho 1-0 Zimbabwe, Cameroon 0-0 Angola, Cape Verde 3-0 Eswatini.