Safari ya kumfurusha Khalwale UDA yaanza akishutumiwa kuunga mwaniaji pinzani Malava
SAFARI ya kumfurusha Seneta wa Kakamega Boni Khalwale UDA imeanza baada ya Kamati ya Nidhamu kumtaka ajibu madai kwa nini asiadhibiwe kwa kuchukua msimamo unaokinzana na chama kuhusu masuala mbalimbali yenye umuhimu.
Bw Khalwale alichaguliwa kama seneta 2022 kupitia UDA na pia ni Kiranja wa Wengi kupitia chama hicho.
Kamati ya nidhamu ya chama inayoongozwa na Wakili Charles Njenga imetaja hatua ya seneta huyo kuendelea kukosoa serikali na kumuunga mkono mwaniaji wa chama kingine katika uchaguzi mdogo wa Malava kati ya sababu ambazo zimesababisha Bw Khalwale ajipate mashakani.
Katika uchaguzi mdogo wa Malava, Bw Khalwale amekuwa akiungana na viongozi wengine wa DAP-K kumpigia debe mwaniaji wa chama hicho Seth Ambusini Panyako.
“Uungwaji mkono wako kwa mwaniaji huyo umekuwa peupe ilhali unafahamu unaenda kinyume na msimamo wa chama,” ikasema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Wakili Njenga.
Chama hicho kiliendelea kumzomea Bw Khalwale, kikimfundisha kuhusu jukumu la seneta na sheria za chama zinavyosisitiza uaminifu kutoka kwa kiongozi yeyote.
“Una siku 14 za kujibu barua hii na iwapo itabainika unastahili kuchukuliwa hatua, basi utaagizwa ufike mbele ya kamati hii,
“Unashauriwa kuwa unaweza kujiwakilisha au kuwakilishwa na wakili na majibu yako yanastahili kuwasilishwa kwa sekretariati ya chama,” ikaongeza barua hiyo.
Katika misururu ya mikutano ya kumpigia debe Bw Panyako, seneta huyo amekuwa akiwaka na kuwaonya wanasiasa kutoka nje dhidi ya kuingilia na kuamua siasa za jamii ya Mulembe.
Pia amekuwa akitofautiana peupe na Rais William Ruto akisema amekuwa akipeleka miradi ya serikali Nyanza na kusahau eneo la Magharibi.
Miezi miwili iliyopita, UDA ilimwandikia aliyekuwa seneta maalum Gloria Orwoba barua kama hiyo kwa kumuunga mkono aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangí.
Bi Orwoba aliishia kufukuzwa kwenye wadhifa wake na nafasi yake ikachukuliwa na Seneta Maalum Consolata Nabwire.