Anayeshukiwa kuua afisa Ikulu azuiliwa kubaini alivyobeba silaha licha ya ulinzi mkali
MWANAMUME anayeshukiwa kumuua kwa mshale afisa wa kikosi maalum cha ulinzi wa Rais karibu na Ikulu ya Nairobi siku ya Jumatatu, atazuiliwa na polisi kwa kipindi cha siku 14 huku uchunguzi ukiendelea, mahakama imeamuru.
Kithuka Kimunyi Musyimi, mwenye umri wa miaka 56, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kibera, Bi Christine Njagi, ambapo aliagizwa azuiliwe korokoroni katika Kituo cha Polisi cha Kilimani.
Akiwa korokoroni, Musyimi atahojiwa kwa kina na maafisa kutoka Kitengo cha Uhalifu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).
Mchunguzi wa kesi hiyo, Inspekta Bashir Boya, alimweleza hakimu kuwa polisi wanahitaji muda wa kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini iwapo Musyimi alishirikiana na watu wengine ambao bado hawajakamatwa, pamoja na sababu ya kufika eneo kama Ikulu akiwa amejihami kwa silaha.
“Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa afisa aliyeuawa, Ramadhan Matanka, ambaye alikuwa mwanachama wa kikosi cha GSU kinacholinda Rais, alikuwa kazini katika Lango D la Ikulu wakati mshukiwa alimvamia akiwa na upinde na mshale aliouficha kwenye gunia,” alisema Inspekta Boya.
Kwa mujibu wa maelezo ya Inspekta huyo, mshukiwa alijificha nyuma ya gari lililokuwa linakaguliwa, akatoa mshale kutoka kwenye gunia na kumpiga Konstebo Matanka kifuani upande wa kushoto, akimsababishia majeraha mabaya.
Mahakama iliambiwa kuwa mshukiwa hana makazi yanayojulikana wala kazi rasmi, na kwa hivyo ni hatari kuachiliwa kwa dhamana kwani anaweza kutoroka na kuhujumu uchunguzi.
“Tuna hofu kuwa akiachiliwa kwa dhamana, anaweza kutoweka,” alisema Inspekta Boya.
Mahakama iliambiwa kuwa uchunguzi umegawanywa katika maeneo matano, ikiwemo kurekodi taarifa za mashahidi, kukagua picha za kamera za CCTV katika Lango D na barabara ya Dennis Pritt, kuchambua mawasiliano ya simu ya mshukiwa, kuchukua alama za vidole na kuziwasilisha kwa kitengo cha kumbukumbu za uhalifu, kumpima hali yake ya akili kabla ya kushtakiwa kwa kosa la mauaji.
Inspekta Boya alieleza kuwa baada ya kukamilisha uchunguzi, faili itawasilishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) apitie ushahidi na kutoa mwongozo kuhusu mashtaka atakayofunguliwa mshukiwa.
Marehemu Matanka alizikwa jana katika kaunti ya Kajiado.
Musyimi, ambaye alionekana kutembea kwa shida na kusaidiwa na maafisa wawili wa polisi, aliomba apelekwe hospitalini akidai alipigwa baada ya tukio hilo.
Alipoulizwa kama alipinga ombi la polisi kumzuilia kwa siku 14, Musyimi hakupinga.
Katika uamuzi wake mfupi, Hakimu Njagi alisema polisi wamewasilisha sababu za msingi za kuendelea kumzuilia mshukiwa.
“Nimepitia ombi na hati ya kiapo ya kuunga kuzuiliwa kwa mshukiwa kwa siku 14. Nimeridhika kuna sababu za msingi. Ombi hili lina mashiko,” alisema Bi Njagi.
Mahakama pia iliagiza mshukiwa kupelekwa hospitalini kupata matibabu na kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 28 2025 ili upande wa mashtaka utoe taarifa kuhusu hali ya uchunguzi.