Akili Mali

Kichujio spesheli kwa ajili ya kuandaa asali safi, iliyo laini

Na RICHARD MAOSI October 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUTENGENEZA bidhaa murwa itakayovutia wateja wengi na warudi tena na tena, asali ghafi hupitia mchakato mrefu kuanzia hatua ya kurina hadi kuipakia kwa mikebe ili kuuzwa sokoni.

Muhimu zaidi katika mchakato huu ni kudumisha usafi wa hali juu tokea mzingani, utayarishaji hadi upakiaji ili kutimiza viwango hitajika vya ubora wa bidhaa inayoliwa na binadamu.

Katika mchakato huu wote mfugaji hutumia vifaa spesheli kwa kila hatua; kama vile honey presser ya kukamua asali kutoka kwa masega, na kichujio cha kuondoa mabaki yoyote ili asali iwe laini.

Mtaalamu wa ufugaji nyuki na mfanyakazi katika kituo cha Bee Farmers Hub jijini Nairobi, Meshack Nzuki, anasema wafugaji wengi humakinikia zaidi hatua ya kwanza ya urinaji – kukata masega mzingani ili kukamua asali.

Hata hivyo, hatua inayofuata ya kuchuja asali hiyo ghafi pia yahitaji umakinifu wa hali ya juu.

“Ikumbukwe kuwa watu hutumia asali sio tu kama lishe bali pia ni dawa. Ila wanachelea kununua bidhaa hiyo kwa kuhofia kwamba huenda imechanganywa na vitu vinginevyo kama vile maji,” anahoji Nzuki.

Meshack Nzuki, mtaalamu wa nyuki na mfanyakazi wa Bee Farmers Hub Nairobi akionyesha mtambo wa double sieve unaotumika kutakasa asali. PICHA|RICHARD MAOSI

Kichujio cha double sieve ni kifaa spesheli ambapo asali hupitishwa kwa vichungi viwili ili kuondoa mabaki yasiyohitajika.

Aidha, hutumia kani ya mashinepewa – yaani nguvu zinazosukuma kitu kwa mwendo wa mviringo unaoelekea nje [centrifugal force kwa Kimombo] ili kutenganisha asali na mabaki mengine yoyote. Mfumo huu umepatikana kuwa faafu zaidi ya mara sita ikilinganishwa na nyenzo za kawaida.

Mabaki hayo hujikusanya sehemu ya chini ya kichujio huku asali safi ikimimina kwa wepesi.

Kifaa hiki husaidia mfugaji kuandaa sio tu asali safi bali pia yenye mtiririko laini – hii ikiwa sifa moja ya kutambua asali bora kwani haifai kushikamana baada ya kupakiwa kwenye mkebe.

“Kifaa hiki kimeundwa kuwarahisishia kazi wafugaji wanaomiliki mizinga mingi na hupata changamoto kuchuja asali ghafi nyinyi kabla ya kuipakia,” alieleza Nzuki.

Mfugaji anatakiwa kuweka kichujio juu ya chombo kitakachotumika kuteka aali safi kama ndoo.

Kisha kifaa kinaunganishwa kwa umeme na kuwashwa huku ukimimina asali.

Unashauriwa kujiandaa vyema kwa asali ghafi nyingi ili kumimina kwa muda bila kukoma, lengo likiwa kuzuia umeme usiwashwe bure.

Vile vile, hakikisha ndoo yako inatoshana na mzingo wa kichujio, ni dhabiti na kubwa ya kuteka asali nyingi ili uendeshe shughuli kwa urahisi katika muda mfupi.

Nzuki anatahadhari kuwa endapo asali ghafi itakuwa na mabaki mengi itakulazimu kuzima kichujio baada ya muda ukisafishe ili tundu ziwe wazi kabla kuendelea na shughuli.