Makala

Nina furaha, naheshimiwa na nalipwa vyema kuliko Kenya, asema afisa anayepigania Urusi

Na NYABOGA KIAGE October 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

AFISA wa zamani wa Kikosi cha Kukabiliana na Fujo (GSU) kutoka eneo la Bonde la Ufa alipanda ndege kuelekea Moscow, Urusi mnamo Julai mwaka jana, akianza ukurasa mpya wa maisha yake, wakati wa vita vikali barani Ulaya.

Leo hii, Kevin (si jina lake halisi) anaongea na Taifa Leo kutoka kambi ya kijeshi kusini mwa Urusi. Licha ya sauti kutosikika vyema, utulivu wake wa moyo ni dhahiri.

“Ninafuraha hapa,” anasema. “Nyumbani kulikuwa hakuna pesa, hakuna fursa. Hapa, ninaheshimiwa, nina lengo, na mshahara ni mkubwa kuliko nilivyowahi kulipwa Kenya.”

Kevin ni mmoja wa Wakenya kadhaa wanaohudumu kwa sasa katika jeshi la Urusi, baadhi kwa hiari, wengine kwa kudanganywa.

Wengine walivutwa na ahadi za mshahara mnono na uraia wa Urusi. Lakini wapo waliodai walihadaiwa kutia saini mikataba kwa lugha wasiyoielewa, wakiamini wanaenda kufanya kazi za kiraia, ila wakajikuta wakifundishwa vita.

Lakini Kevin anasema alijua vyema alichokuwa anakwenda kufanya.

“Nilipoondoka Kenya Julai, nilijua nitajiunga na jeshi la Urusi. Nililikubali jambo hilo,” anasema. “Hadi sasa mambo ni shwari. Nimepanga hata kuongeza mkataba wangu.”

Anasema analipwa Sh316,000 kwa mwezi, kiasi karibu mara tatu ya kile alichokuwa akipata akiwa katika vikosi vya usalama Kenya.

Anadai hajawahi kupigana mstari wa mbele; kazi yake ni kusafirisha chakula kwa wanajeshi na kubeba miili ya waliouawa vitani.

“Nimesikia hadithi za kupotosha,” anaongeza. “Tulipoondoka Kenya, tuliambiwa kuwa tutahusishwa na vita. Kwa nini mtu aseme alidanganywa?”

Kabla ya kujiunga na Urusi, Kevin alihudumu katika maeneo hatari Kenya kama vile Tana River, Baragoi, Pokot Magharibi, Turkana na mpakani mwa Kenya na Somalia.

Anasema maisha ya askari Kenya yalikuwa magumu mno, na Urusi inampa heshima na ujira alioutamani daima.

“Sioni sababu ya kurudi Kenya na kuacha kazi hii. Mwisho wa siku, tunatafuta pesa tu,” anasema.

Lakini si Wakenya wote waliokuwa na ufahamu wa kilichowakabili.

Katika mtaa wa Seasons, Kaunti Ndogo ya Kasarani, Nairobi, kijana mwingine anasema alihadaiwa na ajenti wa kampuni ya usafiri.

Alielezwa kuwa angepata kazi nzuri katika kampuni ya teknolojia ya habari (IT) Urusi.

“Nilitoka Kenya Septemba 15, 2025, nikiamini nitafanya kazi ya IT,” anasema. “Nililipa Sh60,000 kwa stakabadhi na kutayarishiwa safari.”

Lakini alipotua Urusi, ukweli ulipambazuka. “Tulijikuta kambini na Wakenya wengine waliotufumbua macho kwamba tunajiunga na jeshi.”

Waliona majeruhi kutoka mataifa mengine ya Afrika walioumia vitani na kubaini ukweli na ndipo walipoelewa uzito wa hali hiyo.

Yeye na wenzake watatu walipanga kutoroka.

“Walitupokonya simu, lakini mimi niliificha,” anakumbuka. “Tulikuwa tukipewa saa moja kila jioni kwenda kununua bidhaa na tuliitumia nafasi hiyo kutoroka hadi Ubalozi wa Kenya.”

Maafisa wa ubalozi waliwapangia usafiri wa teksi kuwachukua na kuwasaidia kurejea nyumbani.

Ajenti huyo alipoulizwa na Taifa Leo, alikana kuhusika, akidai kutambuliwa kimakosa.

Hata hivyo, mke wa kijana huyo alithibitisha kuwa tayari amewasilisha malalamishi dhidi ya ajenti huyo na kampuni yake bila mafanikio.

“Walikamata watu wasiohusika na kumwacha mtuhumiwa mkuu huru,” alisema. Alidai kuwa mume wa ajenti huyo ni afisa wa cheo cha juu wa DCI, na hivyo amekuwa akimlinda.

Ripoti kuhusu Wakenya kupigana ndani ya jeshi la Urusi zilianza kuibuka mwishoni mwa mwaka jana.

Kwa mujibu wa duru za kidiplomasia, Wakenya kadhaa wamepatikana maeneo ya Urusi au Ukraine yaliyo chini ya Urusi.

Wengine wamejisalimisha kwa majeshi ya Ukraine, huku wengine wakirudishwa nyumbani kupitia juhudi za mashirika ya kibinadamu.

Wizara ya Mambo ya Nje Kenya (MOFA) imethibitisha kuwa inafahamu kuhusu mtandao unaowasajili Wakenya kwa madai ya kazi katika sekta ya uchukuzi lakini hatimaye huwapeleka vitani.

Katibu Dkt Korir Sing’oei amethibitisha kuwa Wakenya 29 wanashikiliwa bila hiari katika mji wa Belgorod, karibu na kambi kubwa ya kundi la Wagner.

“MOFA ipo katika mazungumzo na maafisa wa Kiev, na tayari tumeibua suala hilo kwa Ubalozi wa Urusi. Maafisa wa Urusi wanakana kuhusika kwa serikali,” alisema Dkt Sing’oei.