Mgao kwa shule: Spika aamuru waziri kufika Bungeni
Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetang’ula, amemwamuru Waziri wa Elimu, Bw Ogamba Migos, kufika mbele ya kikao cha Bunge la Taifa leo alasiri kuelezea kwa nini shule hazijapata mgao.
Spika Wetang’ula alisema kuwa ahadi zinazotolewa mbele ya Bunge la Taifa haziwezi kupuuzwa.
Bw Wetang’ula alimwagiza Kiongozi wa Wengi Bungeni, Kimani Ichung’wah, kuhakikisha kuwa Waziri Migos anafika mbele ya Bunge leo Jumatano alasiri kujibu maswali yaliyoibuliwa na Wabunge kuhusu kutotolewa kwa fedha za mgao kwa shule.
Wakati wa mjadala huo, Wabunge walitaka uwajibikaji kutoka kwa Mawaziri ambao, kwa maoni yao, huchukulia kwa mzaha masuala yanayowasilishwa bungeni.
Walisisitiza kuwa ni lazima kuwe na mtu wa kuwajibika kuhusu ahadi ambazo hazijatimizwa na Baraza la Mawaziri.
Mbunge wa Marakwet Mashariki, Bowen David, alisema kuwa mgao kwa shule unapaswa kuzingatiwa kama matumizi ya mara kwa mara ya lazima.
“Waziri wa Elimu alikuwepo hapa wiki iliyopita na akaahidi kuwa fedha za wanafunzi zote zitatolewa. Kwa nini ahadi hiyo haijatimizwa?” aliuliza Bowen.
Bowen aliitaka Kamati ya Bajeti kulichukulia suala hilo kama jambo la kipaumbele.
“Litazameni hili kama hitaji la dharura. Toeni fedha hizi kama tunavyolipwa mishahara yetu na ya watumishi wengine wa umma. Wanafunzi wanateseka, watoto wanahangaika.”
Mbunge wa Gilgil, Martha Wangari, alionya kuwa kunaweza kuwa na kashfa inayonuka katika Wizara ya Elimu.
“Kuanzia wiki ijayo, wanafunzi wa kidato cha pili na cha tatu wanatarajiwa kuruhusiwa kwenda nyumbani; hivyo basi, fedha zitakazotolewa zitatumika kwa matumizi gani?” alihoji.
Waziri wa Elimu alikuwa bungeni wiki iliyopita, ambapo aliahidi kushughulikia mgomo wa wahadhiri wa vyuo, kutoa fedha za mgao, na kutatua matatizo mengine katika wizara hiyo, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa hadi sasa.
Kiongozi wa Wengi Bungeni, Kimani Ichung’wah, alisema kuwa Bunge lina wajibu wa kusimamia kwa makini Serikali kuu.
“Mawaziri wanapofika mbele ya Bunge au Kamati zake, hufanya hivyo kujibu maswali kutoka kwa Wabunge.”
Alisema: “Yale ambayo Waziri anatangaza bungeni ni lazima yatimizwe. Kama Waziri wa Elimu hakumaanisha alichosema, basi hajachukua kazi yake kwa uzito unaostahili. Ni jukumu lake kueleza changamoto anazokumbana nazo.”
Kimani alisema atawasiliana na Waziri wa Elimu kuhusu sababu ya kutotolewa kwa fedha za mgao kwa shule.
“Iwapo ilikuwa ni changamoto ya uhakiki, basi angalau sehemu ya fedha hizo ingetolewa kwa shule,” alisema.
Aliongeza kuwa Waziri hakupaswa kutoa ahadi ambazo hawezi kutimiza.
“Iwapo changamoto ziko Hazina Kuu, jambo ambalo nalitambua, basi alipaswa kueleza hilo. Mawaziri wanapaswa kuchukulia kwa uzito jukumu lao. Ahadi wanazotoa ni kwa wananchi wa Kenya, si kwa Wabunge pekee.”