Nyasi hii ya miujiza kuongeza uzalishaji wa maziwa
MIAKA michache iliyopita, Profesa Joseph Ngugi Kamau ambaye ni mhadhiri wa United States International University (USIU), alinunua ng’ombe wa hadhi wa maziwa ili kumtunuku mama yake anayeenzi sana ufugaji.
Ng’ombe huyo, Prof Ngugi anasema, alipaniwa kumuongezea pato.
Hata hivyo, hakushawishika kwamba mama yake angemudu kumtunza kwani alikuwa angali mateka wa mbinu za zamani kufanya ufugaji.
“Alikuwa ng’ombe wa bei ghali na nilimpa kama zawadi,” anasema mhadhiri huyo anayefunza Ujasiriamali na Masuala ya Ubunifu kwenye biashara katika Chuo Kikuu cha USIU.

Baada ya miezi miwili, aliporejea nyumbani eneo la Maragua, Kaunti ya Murang’a, alishangaa kugundua kuwa mama yake alikuwa ameshamuuza kwa bei anayotaja kama ya “kutupa”.
“Alimuuza kwa bei ya kutupa ya Sh2,000 kwa sababu alisalia kwa mbinu za zamani kumlisha hivyo basi akakosa kumpa maziwa. Isitosha, aliugua akahofia angefariki na akauzia mhudumu wa buchari,” anakumbuka.
Tukio hilo, pamoja na kumbukumbu zake za utotoni – kutembea zaidi ya kilomita mbili kutafutia ng’ombe majani, lilimfanya aone umuhimu wa njia bora za malisho.
Hali hiyo ya mbinu za jadi kufanya ufugaji, anaeleza, si endelevu tena hasa kutokana na gharama ya juu ya chakula cha mifugo cha madukani na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazokumba wafugaji nchini.

Ni kwa sababu hiyo Prof Ngugi amezindua eneo la Maragua ukuzaji wa nyasi ya Juncao, maarufu kama “nyasi ya miujiza”, akiwa na lengo la kubadilisha taswira ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa Murang’a na maeneo mengine.
Nyasi hii ilianza kukuzwa Kenya mwaka 2021, baada ya kuidhinishwa na asasi za utafiti ikiwemo KEPHIS na tayari imepokelewa vyema na wakulima katika kaunti za Nakuru, Turkana, Garissa, Kajiado na Makueni kama njia mbadala kukabiliana na kero ya gharama ya chakula cha mifugo.
Kulingana na wataalamu, Juncao ina protini ghafi ya asilimia 18 ikilinganishwa na Napier ya kawaida yenye asilimia 10 pekee.
Nyasi hii inaweza kustawi eneo lolote lile, ikiwemo eneo kame na nusu kame (ASAL), jambo linaloifanya kuwa tegemeo hata wakati wa kiangazi.
Prof Ngugi kwa sasa ana ekari mbili za nyasi hii Maragua na anasambaza mbegu za kupanda kwa wakazi. Mbegu zake – ni matawi yenye nodi mbili, yaani nodes kwa lugha ya Kiingereza.

“Juncao kwenye ekari moja inaweza kuzalisha hadi tani 10 kwa mwaka, chakula kinachoweza kulisha zaidi ya ng’ombe 20 au mbuzi 200 kwa mwaka mzima,” anafafanua.
Teknolojia ya Juncao ilivumbuliwa miaka ya themanini (1980’s) nchini China na Prof Lin Zhanxi, ambaye ni mhadhiri wa Fujian Agriculture and Forestry University (FAFU), chuo kilichoko nchini humo.
Uvumbuzi wake ulilenga kuzuia uharibifu wa miti ambapo Juncao ilitumika kusaidia kukuza uyoga (mushroom substrate), kuzuia mmomonyoko wa udongo, na baadaye kubainika kuwa ni chakula faafu cha mifugo, hivyo kusaidia pakubwa kuondoa lindi la umaskini.
Wapo wakulima waliojaribu nyasi hii ya miuza, kama Sammy Kariuki kutoka Nakuru, na anasema ng’ombe wake sasa wanazalisha maziwa mara dufu ikilinganishwa na hapo awali.
“Nilianza kulima Juncao 2022, na nimeona mabadiliko makubwa kiuzalishaji maziwa,” Kariuki anakiri.

Ng’ombe aliyekuwa akimpa lita tano za maziwa kwa siku, sasa anadokeza kwamba anampa lita 12.
Prof Ngugi anapiga stamu kauli ya mkulima huyo. “Uzalishaji umeongezeka kwa kati ya asilimia 40 hadi 50,” anathibitisha.
Mbali na kulisha ng’ombe, nyasi hii pia hutumika kwa mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku na hata kutengeneza vipandio vya uyoga. Hali kadhalika, inasaidia kuboresha udongo kwani imesheheni virutubisho vya Kaboni.
Prof Ngugi analenga vijana na wanawake, akisema wana nafasi kubwa kunufaika kupitia biashara ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa kuwa Juncao ni teknolojia ya mambo leo.
“Ni teknolojia ya kisasa inayoweza kubadilisha sekta ya ufugaji na kufanya kilimo kiwe chenye faida tele,” anasema.

Upanzi wake si tofauti na ule wa mahindi na mimea mingineyo.
Mbegu – matawi yenye nodi mbili hupandwa kwa kulalisha na kuhakikisha nodi moja inazikwa udongoni.
Vipimo, ni sentimita 50 kati ya mimea na vilevile kati ya laini ya mimea.
Inakuwa tayari kulisha mifugo baada ya miezi mitatu au minne, na miezi minane kwa mbegu za kuendeleza uzalishaji, Juncao ikisifiwa kudumu shambani karibu miaka 25 kabla ya kuing’oa kupanda nyingine.